Serikali kusitisha matumizi ya kuni

SERIKALI imetangaza kusitisha matumizi ya kuni na mkaa kwa taasisi za umma na binafsi za Tanzania Bara zinazoandaa chakula na kulisha watu zaidi ya 100 kwa siku ifikapo Januari 31, 2024.

Sambamba na hilo, imezielekeza taasisi zinazoandaa chakula na kulisha watu zaidi ya 300 kusitisha matumizi ya kuni na mkaa ifikapo Januari 31, 2025.

Akitangaza uamuzi huo wa serikali, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira na Muungano, Dk Seleman Jafo alisema taasisi hizo zitatakiwa kutumia nishati mbadala ambayo ni safi kwa ajili ya kupikia.

“Natoa katazo hili kwa taasisi hizi kwa mamlaka niliyopewa chini ya Kifungu cha 13 cha Sheria ya Usimamizi wa Mazingira Sura ya 191,” alisema.

Dk Jafo alifafanua kuwa serikali imeweka nia ya kupunguza athari za kimazingira, kiafya, kijamii na kiuchumi zitokanazo na matumizi ya kuni na mkaa kwa kupikia na tayari imeandaa Dira ya Taifa ya Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia pamoja na Mpango Mkakati wa Utekelezaji wa Dira hiyo kwa kipindi cha miaka kumi hadi kufikia 2033.

“Pamoja na urahisi na unafuu wa upatikanaji wa nishati hizi, matumizi yake yanaathiri afya ya mtumiaji kwa kusababisha magonjwa yatokanayo na kuvuta hewa chafu ambayo huathiri mapafu, moyo na magonjwa ya kupumua kwa watoto,” alisema.

Aidha, Dk Jafo alieleza kuwa kipaumbele cha serikali ni kujenga uchumi wa viwanda, hivyo matumizi ya nishati mbadala yatatoa fursa ya viwanda vya kutengeneza mkaa mbadala na kuzalisha majiko sanifu na banifu kwa ajili ya matumizi fanisi ya nishati hiyo.

“Ripoti ya tatu ya hali ya mazingira nchini ya mwaka 2019, inaonesha kuwa kasi ya uharibifu wa misitu ni kubwa na kila mwaka zaidi ya hekta 469,420 huharibiwa kutokana na ukataji wa miti kwa ajili ya matumizi ya kuni na mkaa,” alisema.

“Inakadiriwa kuwa asilimia 16 ya ardhi imeharibika na inakabiliwa na kuenea kwa hali ya jangwa na ukame kutokana na watu wengi kufanya shughuli zisizoendelevu ikiwemo kutumia nishati ya kuni na mkaa kwa ajili ya kupikia,” alisema.

Habari Zifananazo

Back to top button