Serikali kutathmini gharama ya vyakula sokoni

Mkutano Mifumo ya Chakula Afrika kufanyika Dar

SERIKALI imeweka wazi kuwa inatambua mwenendo wa gharama ya chakula sokoni na hivyo inaendelea kufanya tathmini kupata uhalisia wa kiwango cha chakula na kuangalia uwezekano wa kuongeza chakula kutoka kwenye ghala la taifa.

Hayo yamebainishwa jana na Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Dk Ashatu Kijaji wakati akifunga maonesho ya tano ya kitaifa ya teknolojia ya madini katika viwanja vya Bombambili mjini Geita.

Alisema wizara yake inashirikiana na Wizara ya Kilimo kuhakikisha mazingira rafiki na wezeshi kwa wakulima waendelee kunufaika na bidhaa zao sambamba na kuhakikisha Watanzania wanapata chakula kwa gharama nafuu.

Advertisement

“Ni ukweli usiopingika kama ambavyo serikali imekuwa ikisema siku zote,  mwaka uliopita hatukupata mvua za kutosha, siyo sisi Tanzania peke yetu lakini na nchi zilizo jirani na sisi hivyo kumekuwa na uhitaji mkubwa wa chakula,” alisema.

Alifafanua: “Tupo kwenye soko huria, wakulima wetu kwa mwaka huu imekuwa ni neema kwao, wameweza kuuza mazao yao ambayo wamekuwa wakizalisha na miaka mingi wamekuwa wakilalamika kuwa na bei ndogo ya bidhaa zao.”

Alisema mwaka huu bei imekuwa nzuri na wameuza kwa kiwango kikubwa. Aliwapongeza wakulima kwa hatua hiyo lakini akasema, serikali inaangalia upatikanaji wa chakula ndani ya taifa  kama chakula kipo na wanaendelea kufanya tathmini ya kiwango cha chakula.

“Sasa tulipofika ni wakati wa kuongeza upatikanaji wa chakula kutoka kwenye maghala ya taifa letu, nitaenda kuyafikisha hayo na ni imani yangu kwa hatua tuliyofikia chakula kitaongezwa kwenye masoko yetu,” alisema.

Katika hatua nyingine, Dk Kijaji alieleza pia serikali inaendelea kuweka mazingira rafiki kuhamasisha uwekezaji wa viwanda nchi nzima ili kuongeza upatikanaji wa bidhaa na kuchagiza ukuaji wa kiuchumi.

Aidha, alizitaka taasisi zote kwenye sekta ya madini na biashara kuimarisha tafiti za teknolojia ili upatikanaji wa malighafi muhimu uwe rahisi kwa wachimbaji na kuongeza mchango wa sekta ya madini uliofikia asilimia 7.2 sasa.

Awali, Mbunge wa Jimbo la Geita Mjini, Costantine Kanyasu aliomba serikali kufanya tathmini na kujua kiini cha kupanda kwa gharama ya chakula na bidhaa mbalimbali na kuwafanya Watanzania kunufaika na fursa zilizopo nchini.

Waziri wa Madini, Dk Dotto Biteko alieleza mchango wa wachimbaji wadogo kwenye sekta ya madini umeimarika kutoka asilimia nne hadi asilimia 40 kutokana na sera rafiki zinazosimamiwa na serikali ya awamu ya sita.

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martin Shigella alisema maonesho hayo yamekutanisha jumla ya washiriki 465 na wamejipanga kuyakuza kwa kuyafungamanisha na biashara ya madini na uongezaji wa thamani wa madini hayo.