Serikali kutathmini meli Mtwara-Comoro

Bandari ya Mtwara.

SERIKALI imesema imetenga fedha kwa mwaka wa fedha 2023/2024 kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu katika Bahari ya Hindi, kwa lengo la kujiridhisha na kiwango cha mahitaji ya usafiri wa meli kwa wananchi wa mwambao wa Pwani ya Bahari ya Hindi na nchi jirani ikiwa ni pamoja na Visiwa vya Comoro.

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Atupele Mwakibete amesema upembuzi huo utasaidia serikali kuamua aina ya meli itakayojengwa kulingana na hitaji la wananchi na soko kwa ujumla. 

“Serikali inatambua umuhimu wa mawasiliano baina yake na mataifa jirani hasa nchi ya Comoro. Serikali kupitia Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL) imetenga fedha,” Naibu Waziri amesema wakati akijibu swali la Mbunge wa Newala Vijijini, Salum Mtanda.

Advertisement

Mbunge huyo alihoji ni lini Serikali itajenga meli katika Bandari ya Mtwara itakayorahisisha mawasiliano na nchi ya Comoro. 

Mwakibete amesema pamoja na hatua hiyo ya kufanya upembuzi yakinifu, Serikali kupitia Mamlaka ya usimamizi wa Bandari imefanikiwa kuishawishi Kampuni ya Meli ya CMA CGM kutumia bandari ya Mtwara kama kitovu (hub) cha mizigo inayokwenda visiwa vya Comoro.

Hivyo, mizigo inayotoka nchi za Ulaya na Asia kwenda Comoro na ile inayotoka Tanzania kwenda Comoro (transshipment) imeanza kuhudumiwa katika Bandari ya Mtwara. 

Meli ya Kampuni ya CMA CGM ilianza safari za kupitia bandari ya Mtwara tarehe 20 Aprili, 2023 na itaendelea kutoa huduma hiyo kila baada ya wiki moja. Aidha, meli ya kwanza kutoka Mtwara kwenda Comoro iliondoka tarehe 02 Mei, 2023 na itaendelea kutoa huduma hiyo kila baada ya wiki mbili.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *