Serikali kutumia tril 1.1/- miradi ya maji Dar, Pwani

SERIKALI kupitia Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira (DAWASA) imewekeza Sh trilioni 1.1 kutekeleza miradi 13 ya majisafi na usafi wa mazingira Dar es Salaam na Pwani.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Cyprian Luhemeja alisema Dodoma kuwa lengo la uwekezaji huo ni kuhakikisha huduma ya majisafi kwa wakazi wa eneo ambalo DAWASA inalihudumia la Dar es Salaam na Pwani inapatikana kwa asilimia 100 huku uondoaji majitaka ufikie asilimia 60 ifikapo mwaka 2023.

Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa mwaka 2021/22 hadi 2025/26 umeweka kipaumbele katika upatikanaji na usambazaji wa majisafi na salama vijijini na mijini na utunzaji wa vyanzo vya maji na mazingira.

Mpango umelenga kuhakikisha asilimia 95 ya idadi ya watu katika Jiji la Dar es Salaam na makao makuu ya mikoa wanapata maji ya bomba au maji yanayolindwa kama chanzo kikuu.

Ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)  imeielekeza serikali kuhakikisha upatikanaji wa maji kwa mijini inakuwa asilimia 95 na vijijini inakuwa asilimia 85 ifikapo mwaka 2025.

Kwa sasa upatikanaji wa huduma ya majisafi ni asilimia 96 kwa Dar es Salaam na Pwani wakati uondoaji wa majitaka ni asilimia 30.

Luhemeja alisema kupitia Mpango Biashara wa DAWASA wa miaka mitatu 2021/2022 hadi 2023/2024, imejiwekea malengo kuhakikisha upatikanaji wa huduma ya maji unafikia asilimia 100 na huduma ya usafi wa mazingira inafikia asilimia 60.

Alisema kwa mwaka 2022/2023 DAWASA inatekeleza miradi ya kimkakati 13 yenye thamani ya Sh trilioni 1.1.

Mradi wa uboreshaji wa mfumo wa usambazaji maji kuanzia Chuo Kikuu cha Ardhi hadi Bagamoyo.

Alisema mradi huo ambao unahusisha kilomita 1,426 na unalenga kusambaza maji kutoka Changanyikeni, Goba, Madale, Mivumoni Mabwepande, Mbweni Mapinga, Vikawe hadi Bagamoyo.

Luhemeja pia alisema umehusisha ujenzi wa matangi matatu ya Tegeta A, Mbweni na Vikawe.

Alisema DAWASA imepanga kutumia Sh bilioni 65 katika mradi huo na Sh bilioni 5 kwa ajili ya mkandarasi mshauri.

Mradi wa maji Mshikamano

Luhemeja alisema mradi huo imelenga kuondoa changamoto ya maji katika kata za Mbezi na Kwembe katika Jimbo la Kibamba. Alisema mradi unahusisha ujenzi wa tangi na ufungaji wa pampu na matarajio utakamilika ifikapo Desemba mwaka huu.

Mradi wa maji Kigamboni

Luhemeja alisema mradi huo unagharimiwa na fedha za ndani na imetengewa Sh bilioni 23 ukihusisha ujenzi wa tangi na kujenga visima saba vyeye uwezo wa kutoa maji lita milioni 60 kwa siku.

“Maji ambayo yatazalishwa kwenye huu mradi ni lita milioni 60 wakati mahitaji ya Kigambani ni lita milioni 25, hivyo kazi pekee itakayobaki ni kusambaza mitaani na nyumba kwa nyumba ambayo tunaamini mwakani kazi hii itakuwa imeshika kasi, na uzuri wa Kigamboni watakuwa na chanzo chao.”alisema.

Mradi wa Chalinze awamu ya tatu

Luhemeja alisema mradi huo utakamilika Oktoba na kufuatiwa na majaribio kabla ya kuanza kutoa huduma Desemba mwaka huu.

Alisema mradi unahusiaha usambazaji wa mabomba, ujenzi wa matangi makubwa na madogo.

“Ni mradi pekee wa mfano ambao unapeleka maji vijijini kwa njia ya bomba na utaunganisha vijiji 74. Ifikapo Desemba mradi huu utaanza kutoa huduma ya maji.”alisema Luhemeja.

Mradi wa Bwawa la Kidunda

Alisema DAWASA inatarajia kuanza kutekeleza mradi wenye thamani ya Sh bilioni 388 wa ujenzi wa Bwawa la Kidunda lenye uwezo wa kuhifadhi lita trilioni 1.6 baada ya kukamilika kwa mchakato wa ununuzi.

Luhemeja alisema katika awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mradi huo Sh bilioni 60 zimetengwa.

“Rais Samia Suluhu Hassan ameshatenga fedha za mradi na Oktoba mkandarasi atakabidhiwa eneo la mradi baada ya kupata idhini za kisheria”alisema na akabainisha kuwa, baada ya miaka minne bwawa likijaa Dar es Salaam itakuwa na neema ya maji hata kama mvua zisiponyesha wa muda fulani.

Mradi wa majisafi ya pembezoni

Luhemeja alisema DAWASA imetenga Sh bilioni 22 kwa ajili ya kusambaza maji pembezoni kama vile Chanika, Chamazi, Pembamnazi, Kyembesamaki na Kizuriuonjwa.

“Dar es Salaam inakuwa kwa kasi, hivyo tumeona tuwe na mtandao rasmi wa mabomba, na sasa mkandarasi yuko na kazi inaendelea hivyo wananchi wa maeneo hayo wasiwe na wasiwasi kazi imeshaanza.”alisema.

Ujenzi wa mtambo wa majitaka Mbezi Beach

Luhemeja alisema DAWASA imetenga Sh bilioni 154 kwa ajili ya kuondosha majitaka kwa kujenga mtambo mkubwa wa kuchakata majitaka Kilongawima-Mbezi beach na mtandao wa majitaka.

“Kutokana na mtambo huo tutajenga mtandao wa majitaka kuanzia kwa Warioba kuja Mbezi beach, Tangibovu, Kunduchi, Kilongawima ambako hakuna mtandao wa majitaka.”alisema.

Mradi wa ujenzi wa mtambo wa majitaka Buguruni

Luhemeja alisema DAWASA pia imetenga Sh bilioni 207 kwa ajili ya kujenga mtambo wa majitaka Buguruni na unatarajia kuanza Oktoba mwaka huu na kwa sasa mamlaka iko hatua za mwisho za kukamilisha masuala ya mazingira ili mkandarasi aanze kazi katika mwaka wa fedha.

“Huu mradi unakwenda kukusanya majitaka yote ya Ilala badala ya kumwaga baharini tunayapeleka kwenye mtambo wa Buguruni. Wananchi wa Masaki, Buguruni na Tabata wanapata huduma hii.”alisema na akaongeza;

“Pia utachukua majitaka kutoka Magomeni, Ada Estate na Oysterbay na eneo la Jangwani tutajenga mtambo mdogo wa kukusanya majitaka halafu tutafunga pumpu itakayokuwa ikisukuma kwenda Buguruni”.

Luhemeja alisema DAWASA pia itatumia Sh bilioni 4.3 fedha za ndani ili kuyachakata na kuyasafisha maji yaliyoko kwenye mabwawa ya majitaka na kuyaelekeza viwandani.

Mradi majitaka Pembezoni 

Alisema DAWASA imetenga Sh bilioni 22 kwa ajili ya kujenga mitandao midogo ya majitaka maeneo ya pembezoni na kazi zinaendelea.

Mradi wa ujenzi wa vituo vya huduma za usafi kwa umma

Luhemeja alisema kupitia mradi huo, DAWASA inajenga vituo 30  vyenye thamani ya Sh bilioni 3.3 kwenye maeneo ya mikusanyiko mfano vituo vya mabasi, hospitali na masoko.

Mradi wa magari ya majitaka

Alisema DAWASA imetenga Sh bilioni 1.2 kwa ajili ya kununua magari ya kuondoshea majitaka hivyo koongeza nguvu ya magari 13 yaliyopo sasa.

“Sisi tutakuwa na ghrama nafuu kutokana na kuwa bei ambayo inapangwa na EWURA itakuwa bei ya Serikali tofauti na watoa huduma binafsi.”

Aidha, Luhemeja aliwataka wananchi kujitokeza kuhesabiwa Ili kazi ya usanifu wa mradi wa kuyatoa maji Rufiji uakisi ididi halisi ya wakati na miaka 10 ijayo. Makadilio ya takwimu za mwaka 2012 ni kuzalisha lita milioni 750.

Ushirikishaji Watanzania 

Alisema miradi ya DAWASA inajumuisha kampuni za kitanzania kwa zaidi ya asilimia 80.

Upotevu wa maji

Luhemeja alisema DAWASA imetenga Sh bilioni 16 kukabili upotevu wa maji na mradi huo umeanza.

“Kiwango cha asilimia 38 kwa majiji kinaonekana kiko chini kwa sababu DAWASA ina mtandao wa kilomita 4,700 huku ikihudumia watu milioni 8.7, lakini hali hiyo hatuwezi kukubali ndio maana tumetenga shilingi bilioni 16 kwa ajili ya kupambana na upotevu wa maji.”alisema.

Luhemeja alisema DAWASA inapimwa kiwango cha maji kwenye eneo la uzalishaji na kuwa kupitia mradi huo wanagawa maeneo na kufunga mfumo utakaofuatilia mtiririko wa maji na kubaini eneo lenye upotevu.

 

 

 

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button