Serikali kuwafutia usajili wazembe sekta afya

DAR ES SALAAM: WAZIRI wa Afya, Ummy Mwalimu amesema serikali haitawafumbia macho watumishi wanaokwenda kinyume na miiko na taratibu za huduma ya afya.

Waziri Ummy ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam, wakati wa Uzinduzi wa Mpango Jumuishi wa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii, katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC).

“Tutawachukulia hatua, ikiwemo kufuta usajili wao wa kutoa huduma ndani ya serikali na nje ya serikali,” amesema Ummy.

Advertisement

Kiongozi huyo pia hakusita kuwapongeza wale wote wanaofanya vizuri katika sekta ya afya kwa kusema hafurahii, kuona watumishi wa afya wanasakamwa kwani wengi wanachapa kazi,

“Niwashukuru sana sana sana watumishi wote wa afya wa ngazi zote. Wanafanya kazi kubwa sana,” amesema waziri huyo.

Amesema viashiria vya kupima hali ya huduma ya afya nchini vinaonesha sekta ya afya inapiga hatua kubwa ijapokuwa kuna changamoto kadhaa.

“Mheshimiwa Makamu wa Rais, hatusemi kwamba changamoto hazipo. Changamoto bado zipo lakini makubwa ambayo tunapambana nayo sasa hivi ni mambo makubwa mawili la kwanza ni ubora wa huduma za afya jambo la pili ni ugharamiaji wa huduma za afya.” Amesema Mwalimu

Amesema kelele zilizopo mtaani zinasababishwa na uwezo mdogo wa watanzania kumudu gharama za huduma ya afya hivyo kupitia utekelezaji wa sheria mpya ya bima kwa wote inaenda kutatua changamoto hizo.