Serikali mbioni kukamilisha utoaji Hadhi Maalumu

DODOMA; SERIKALI imesema ipo katika hatua za kukamilisha kutoa Hadhi Maalumu kwa raia wa nchi nyingine wenye asili ya Tanzania.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba, akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara yake kwa mwaka wa fedha 2024/25 mjini Dodoma leo, amesema kutolewa kwa hadhi hiyo kutawezesha raia hao kunufaika na baadhi ya haki na upendeleo kutokana na asili yao.

“Naomba sasa nitumie fursa hii kulijulisha Bunge lako tukufu kuwa, Serikali ipo katika hatua za kukamilisha kutoa Hadhi Maalumu (Special Status) kwa raia wa nchi nyingine wenye asili ya Tanzania (Tanzania Non- Citizen Diaspora), ambapo itawasilisha katika Bunge hili muswada wa marekebisho madogo ya Sheria za Uhamiaji Sura ya 54 na Sheria ya Ardhi Sura ya 113 ili kuwezesha utekelezaji wake.

Isome pia:https://habarileo.co.tz/diaspora-wamwaga-fedha-uwekezaji-tanzania/

“Kutolewa kwa hadhi hiyo kutawezesha raia hao kunufaika na baadhi ya haki na upendeleo kutokana na asili yao.

“Aidha, hatua hii pia itawezesha Taifa kunufaika zaidi katika maeneo mbalimbali ya kisekta ikiwemo kupokea fedha za kigeni, ujuzi adimu, uwekezaji, kutangaza utalii, kubidhaisha Kiswahili; kuchochea fursa za Uchumi wa Buluu na manufaa mengine kwa ndugu, jamaa na marafiki,” amesema Waziri Makamba.

Habari Zifananazo

Back to top button