Serikali mbioni kutangaza ajira mpya 47,000
GEITA: Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene amesema serikali imepanga kutangaza ajira mpya takribani 47,000 ili kupunguza uhaba wa watumishi.
Waziri Simbachawene ametoa taarifa hiyo wakati akizungumuza na watumishi wa umma wilayani Chato mkoani Geita na kueleza uhaba wa watumishi unatokana na ujenzi wa miundombinu unaoendelea.
Simbachawene ameeleza, katika kuendelea kukabiliana na uhaba wa watumishi wa kada tofauti kwenye ofisi za umma hadi mwezi Agosti 2023 serikali ya awamu ya sita imefanikiwa kutoa ajira kwa watumishi 129,074.
Amesema serikali pia imepandisha vyeo watumishi 455,497 tangu ilipoingia madarakani mwezi Februari mwaka 2021 hadi Agosti 2023 na kufanya gharama za serikali kufikia Sh bilioni 84.3 kwa mwezi.
Amebainisha kwa mwaka 2022 pekee watumishi 145,225 walipandishwa madaraja kati ya watumishi wa serikali 544,714 waliopo kwenye mfumo pasipo kujumuisha watumishi wa mikataba na vyombo vya ulinzi.
“Kwa upande wa ubadilishaji wa kada, wamebadilishwa kada watumishi 4,866 huku malimbikizo ya mishahara takribani shilingi milioni 220.12 zimelipwa ambazo zimekwenda kwa watumishi 130,116.