WIZARA ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imepanga kujifungia kwa siku tatu na wadau wa elimu wakiwamo wanazuoni kujadili maoni kuhusu mitaala na mapitio ya sera ya elimu.
Mkutano huo utafanyika jijini Dodoma kuanzia Jumatatu hadi Septemba 28 mwaka huu ukijumuisha wahadhiri, waajiri, wadau wa maendeleo, taasisi za umma na binafsi, taasisi za dini, taasisi za uendeshaji wa lugha, wabunge na timu ya Zanzibar inayoshughulikia sera na mitaala.
Wanazuoni wengine ni makamu wakuu wa vyuo vya elimu ya juu vya umma na binafsi, maofisa elimu mkoa na wadhibiti ubora wa elimu.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda alisema wadau watakuwa na kujumu ya kupitia maoni ambayo yamepokelewa hadi sasa.
“Kesho (leo) tutakuwa na majadiliano ya ndani na jumuia za kitaalamu, taasisi za sayansi na utafiti, tunataka kupitia rasimu ambazo tunazo sasa hivi,” Profesa Mkenda aliwaeleza waandishi wa habari Dodoma.
Aidha, alisema ingawa suala la elimu si la Muungano, lakini wanawashirikisha wataalamu kutoka Zanzibar.
“Tumekusanya maoni mengi na mengine yanakinzana, hivyo tumeamua tuwalete wadau wa elimu kwa pamoja tunataka tukae nao tuonyeshe kwamba baada ya kukusanya maoni tunacho hiki na tutawagawia rasimu ya mitaala na mapitio ya sera mapema,”alisema profesa Mkenda.
Aliongeza “Tutajifungia kuona namna gani tunapata rasimu ambayo ina muafaka mkubwa zaidi na muda wowote kati ya mwezi Oktoba na Novemba tutakuwa na kongamano la elimu la siku tatu na tutaweka hadharani rasimu zote.”
Profesa Mkenda alisema lengo la Wizara ni kuhakikisha ifikapo Desemba rasimu ya mitaala na ile ya mapitio ya sera ziwe tayari kwa ajili ya mchakato wa uamuzi.
Aidha, Profesa Mkenda alisema wamezindua tuzo za waandishi bunifu zijulikanazo kama tuzo za Mwalimu Nyerere.