Serikali, wadau kupunguza tatizo la ‘watoto wa mitaani’

WIZARA ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu imejipanga kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha inapunguza tatizo la watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Zainab Chaula wakati akizungumza katika kikao na Taasisi ya Azaria Foundation jijini Dodoma.

Dk Chaula alisema jamii inapaswa kuwa na upendo ili kuhakikisha watoto wanatunzwa katika familia ili wapate malezi na makuzi bora katika ukuaji wao.

Dk Chaula alisema pamoja na kuwa mwanzilishi wa taasisi hiyo ni zao la watoto walioishi mazingira magumu baada ya kutelekezwa na familia yake amekuwa msaada kwa watoto wengine ili wasiendelee kuishi maisha hayo.

Naye Mkurugenzi na Mwanzilishi wa Taasisi ya Azaria Foundation, Audax Abeli ambaye ameishi maisha ya mtaani alisema familia yake ilikuwa chanzo cha yeye kuitwa mtoto wa mtaani jina ambalo siyo sahihi hivyo namna bora ya kuwatoa watoto hao mtaani ni kuanzia upendo kwao.

Hadi sasa taasisi hiyo inahudumia jumla ya watoto 70 kwa kuwapatia huduma muhimu za kijamii na kuwapatia mbinu mbadala za kupambana na maisha.

Kwa upande wake, Kamishna wa Ustawi wa Jamii kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Nandera Mhando alisema wizara itashirikiana vyema na mdau wa taasisi hiyo kushughulikia watoto wanaoishi mazingira magumu na kuwatoa mtaani.

 

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button