DAR ES SALAAM: Serikali kupitia Wizara ya Afya itaendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo ili kuhakikisha kuwa huduma bora za afya zinapatikana kwa watanzania wote.
Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dk John Jingu Machi 7, 2024 kwenye hafla ya kufunga programu ya BACKUP Health jijini Dar es Salaam.
Programu hiyo ya miaka mitatu iliyopo kwenye nchi za Afrika takriban 6 ikiwemo Tanzania, DRC, Mozambique Zimbabwe, Nigeria na Uganda, ni mradi uliyo gharimu euro milioni 20 ambapo kwa Tanzania euro million 3 zimetumika kwenye utekelezaji kwa kupitia ufadhili wa Serikali ya Uingereza FCDO (Foreign commonwealth and Development Office) na kutekelezwa na Serikali ya Ujerumani kupitia GIZ (German Development Cooperation).
Katika hotuba yake, Dk Jingu ameelezea mafanikio ya programu hii katika kuimarisha mifumo ya afya nchini Tanzania. Amesisitiza azma ya serikali ya Tanzania katika kuendelea kufanya kazi na wadau wa maendeleo ili kuhakikisha kuwa huduma bora za afya zinapatikana kwa watanzania wote, hata baada ya kumalizika kwa programu hiyo.
Kwa upande wake Kiongozi wa Programu kutoka GIZ German Cooperation, Huzeifa Bodal ameeleza jinsi programu hii imesaidia kuboresha ufanisi wa huduma za afya, kushirikiana na jamii, na kuongeza ushirikiano kati ya serikali na vituo vya afya na kutoa taarifa kuhusu mchango wa Ujerumani katika kuboresha mifumo ya afya ya Tanzania, akisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa katika kufanikisha malengo haya.