SERIKALI imekutana na wakulima wa zao la vanila mkoani Dodoma, ambapo wameweka mkakati wa pamoja wa kuinua zao hilo.
Naibu Waziri wa Kilimo, Anthony Mavunde ameyasema hayo leo Aprili 18, 2023 Bungeni mjini Dodoma.
Amesema tayari wametengeneza mwongozo kuhusu mfumo wa bei, masoko, na uzalishaji bora wenye viwango wa zao hilo.
“Kwa upande wa masoko, tayari tumeshamwandikia Balozi wa Tanzania nchini China, ambao ndio wanunuzi wakubwa, na tunaendelea kufanya hivyo kwa balozi zetu nyingine,” amesema
Mavunde ameyasema hayo akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Bernadetha Mushashu, aliyehoji ni lini serikali itatafuta soko la uhakika la zao la Vanila?
Aidha, Mavunde amesema serikali kwa kushirikiana na wadau wa sekta binafsi inatekeleza mikakati mbalimbali ili kuhakikisha wakulima wakiwemo wa zao la vanilla wanapata soko la uhakika.
“Mikakati hiyo ni pamoja na kuhamasisha kilimo cha kibiashara kinachozingatia mahitaji ya soko, kushiriki makongamano na maonesho ya kibiashara na uwekezaji, ujenzi wa miundombinu ya masoko na kuimarisha mifumo ya kielektroniki ambayo itasaidi upatikanaji wa taarifa za masoko,”amesema.
Amesema, Serikali inahamasisha sekta binafsi kuwekeza katika uongezaji thamani wa zao la vanilla, ili kupanua wigo wa soko la zao hilo.
“Wakulima wa vanilla wanahimizwa kuvuna vanila zilizokomaa ili kukidhi mahitaji ya soko hususani vanillin isiyopungua asilimia 1.8 na unyevu wa wastani wa asilimia 25 hadi 30,” Amesema