SERIKALI imesema Watanzania takribani 210 waliopo Sudan wakiwamo wanafunzi 171 wapo salama.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Stergomena Tax amesema hayo bungeni Dodoma jana wakati akilitaarifu Bunge kuhusu hali inavyoendelea katika Jamhuri ya Sudan.
Dk Tax amesema serikali imeendelea kuwasiliana mara kwa mara na Ubalozi wa Tanzania uliopo Khartoum ili kuelewa hali inavyoendelea na hadi sasa hakuna Mtanzania aliyeripotiwa kuathiriwa na mapigano hayo.
“Serikali inawahakikishia Watanzania kwamba inachukua hatua stahiki kwa kushirikiana na nchi jirani, Jumuiya za Kikanda, Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa, ili kuhakikisha kuwa Watanzania waliopo nchini humo na raia wengine wanakuwa salama,” alisema Dk Tax.
Dk Tax aliwaeleza wabunge kuwa Aprili 15, mwaka huu yalizuka mapigano kati vikosi vya Serikali (SAF) na Vikosi vya Usaidizi wa Jeshi (RSF) katika Mji Mkuu wa Sudan, Khartoum na katika maeneo mengine nchini humo.
Alisema taarifa zinaonesha mapigano hayo yamesababisha vifo 185, majeruhi zaidi ya 1,000 na uharibifu wa mali ikiwa ni pamoja na ndege.
Dk Tax alisema mapigano hayo yamechangia kurudisha nyuma jitihada za kutafuta amani nchini Sudan na kwamba serikali inasikitishwa na hali ya kuzorota kwa amani na usalama na imeendelea kufuatilia hali hiyo.
Bunge limeelezwa kuwa kwa kuwa Tanzania ni mjumbe wa Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika, inaunga mkono tamko la Baraza la Amani na Usalama la AU katika mkutano wake wa 16 Aprili, 2023 lililolaani mapigano yanayoendelea Sudan na inatoa mwito kwa pande zote katika mgogoro huo kusitisha mapigano yanayoendelea.
“Tanzania inazitaka pande mbili zinazohasimiana kutatua mgogoro huo kwa njia ya amani huku zikihakikisha mahitaji ya kibinadamu, usalama na ustawi wa raia wa Sudan na raia toka nchi nyingine,” alisema Dk Tax.
Alisema juhudi zinazofanywa na Tanzania kwa kushirikiana na jumuiya za kimataifa, ziliwezesha mapigano kusitishwa kwa saa 24 kuanzia Aprili 18 saa 10:00 jioni kutoa fursa za mahitaji ya kibinadamu.
Dk Tax alisema kuna mwelekeo wa kusitisha mapigano na kuruhusu njia za kutatua mgogoro huu kwa amani, na serikali inaendelea kufuatilia na kuandaa mipango ya kuwachukua raia wa Tanzania kadri itakavyohitajika.
Juzi Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ilitoa taarifa kulaani mapigano yanayoendelea nchini Sudan na ikatoa mwito kwa pande zinazopigana kusitisha mapigano.