CHUO Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), kimeipongeza serikali ya wanafunzi chuoni hapo kwa kutumia zaidi ya sh milioni 60 kwa ajili ya kulipia ada wanafunzi, kununua jenereta, kompyuta na mashine za photocopy kwa ajili ya kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wanafunzi wa chuo hicho.
Pongezi hizo zimetolewa na Makamu Mkuu wa OUT, Profesa Elifas Bisanda katika kikao cha 42 cha Bunge la wanafunzi wa chuo hicho kilichofanyika mkoani Manyara.
Profesa Bisanda amesema serikali ya wanafunzi imekuwa ikijitahidi kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wanafunzi kwa kushirikiana na uongozi, pamoja na walimu ili kuwawezesha wanafunzi wawe katika mazingira bora.
Kwa upande mwingine amesema chuo hicho kimekuwa kikilipa sh billion 1.3 kila mwaka, kwa ajili ya matumizi ya intanet, lakini bado haitoshi, na serikali imewaahidi kuingiza mkongo wa taifa katika vituo vyake vyote.
Awali Rais wa serikali ya wanafunzi (OUTSO), ambaye ni Spika wa Bunge la Wanafunzi, Felix Lugeiyamu amesema bunge hilo linashukuru kwa uhusiano mzuri uliopo kati ya menejimenti na serikali ya wanafunzi.

Amesema wamefanikiwa kununua jenereta katika mkoa wa Mara, mashine za photocopy na kompyuta katika vituo vya Pemba, Songwe, Pwani, Geita na kutoa sh milioni tatu kwa wabunge waliopo kila mkoa, ili kuratibu shughuli za kibunge.
” Tukishirikiana kwa pamoja uongozi, wanafunzi na walimu chuo kitafika mbali sana. Tunafanya hivyo kuhakikisha tunatengeneza mazingira bora kwa wanafunzi,” amesema.
Kwa upande mwingine amesema serikali hiyo kwa miaka miwili ya masomo iliyopita, wameweza kulipia wanafunzi 68 waliokuwa wamekwama kuendelea na masomo kiasi cha Sh milion 36.5.
Amesema mwaka huu wamepanga kulipia ada wanafunzi 27 kiasi cha Sh milioni 11.6.