SERIKALI imeagiza kila mkoa kuhakikisha unaanzisha kampeni maalumu yakutengeneza mazingira ya ukijani kwa kuweka mikakati madhubuti ya kurejesha uoto wa asili nchini.
Naibu Waziri wa Utalii ametoa maagizo hayo leo Novembe 22, 2022 wakati akizindua warsha ya urejeshaji wa uoto wa asili (AFR100) iliyowakutanisha wadau mbalimbali wanaotekeleza shughuli za uhifadhi lengo likiwa ni kujenga msingi wa kuandaa taarifa za pamoja ya nchi ya utekelezaji wa makubaliano ya nchi kurejesha uoto wa asili iliyoyafanya mwaka 2018.
Waziri wa Utalii wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja akiwa na wadau mbalimbali wa sekta ya utalii
Masanja ameeleza kuwa tayari kampeni hiyo inafanywa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania – TFS katika mkoa wa Dodoma na kuonyesha mafanikio makubwa kwa kujulikana kama Dodoma ya kijani na kwamba sasa imefika wakati ianze kufanyika katika mikoa yote nchini.
Amesema kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo zinashirikiana na nchi zingine kuhifadhi misitu yake ambapo hadi kufikia mwaka 2030 inatakiwa iwe imerejesha uoto wa asili katika eneo la hekta milioni 5.2.
Katika kufikia lengo hilo, Masanja ameshauri kuwa kuna haja ya kila mkoa kuanzisha kampeni hiyo ya kuwa na ukijani wake ambayo itatokana na kuweka mikakati madhubuti ya kutunza mazingira na kurejesha uoto wa asili.
“Tanzania ni miongoni mwa nchi 54 zilizoingia kwenye mkataba wa urejeshaji wa uoto wa asili ambao kati ya hizo, tayari nchi 32 zimesaini mkataba na kuingia katika utekelezaji wa uoto huo…
…Malengo ya dunia ni kuhakikisha kwamba jumla ya hekta milioni 350 zinarudi kwenye uoto wa asili, kwa Afrika tuna malengo ya jumla ya hekta milioni 100 ambazo zinatakiwa kurejeshwa kwenye uoto wa asili. Tanzania tumejiwekea malengo ya kurejesha uoto huo wa asili kwa hekta milioni 5.2 mpaka kufikia mwaka 2030.”amesema Masanja.
Kamisha wa Uhifadhi TFS, Prof. Dos Santos akizungumza kwenye Warsha hiyo
Kamisha wa Uhifadhi TFS, Prof. Dos Santos Silayo anasema katika kufanikisha hilo la kurejesha uoto wa asili wanahakikisha maaeneo ya misitu yaliopo nchi kavu na baharini sambamba na maeneo ambayo yana mito na uoto wa misitu hayaharibiwi.
“Na hata yale ambayo yameharibika kutokana na shughuli mbalimbali za kibinadamu, iwe ni uvamizi kwa ajili ya makazi, shughuli za uvunaji wa nishati ya mkaa na nyinginezo, kuhakikisha yanarejesha uoto wake wa asili kwa kupanda miti katika maeneo yote ambayo yameharibika na hata katika maeneo mengine ambayo hayajaharibiwa ili kutoa mbadala wa mazao ya misitu katika maeneo hayo,” amesema Prof. Silayo…
…Katika kufanikisha hili, wadau mbalimbali wanatakiwa kushiriki ikiwamo wananchi, serikali, mashirika na asasi za kiraia. Na mkakati huu unalenga siyo kuboresha mazingira yaliyoathirika, lakini kuhakikisha kwamba jamii zinazoishi katika maeneo mbalimbali zinanyanyuliwa kiuchumi.” ameongeza Prof. Silaya.