WIZARA ya Maliasili na Utalii, imeagiza kufanyika upya tathmini ya maeneo mbalimbali yaliyopandishwa hadhi kuwa mapori ya akiba, yapatayo matano Mikoa ya Katavi, Kigoma na Tabora, baada ya malalamiko kutoka kwa viongozi na wananchi wa maeneo hayo kuhusiana na mwingiliano wa mipaka.
Agizo hilo lilitolewa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Maryprisca Masanja katika ziara ya siku moja aliyoifanya mkoani Katavi Jumamosi Septemba 10, 2022.
Amesema baada ya kutoka kwa matangazo ya kupandisha hadhi baadhi ya maeneo tengefu kuwa mapori ya akiba Juni 2021, yaliibuka malalamiko ya baadhi ya maeneo ya mamlaka za serikali za mitaa, vikiwemo vijiji na maeneo mengine kuingizwa ndani ya mapori hayo ya akiba.
Masanja alieleza kuwa baada ya malalamiko hayo, Wizara ya Maliasili na Utalii, iliunda kamati ya wataalam kwa kushirikiana na Mamlaka ya Usimamizi wa wanyamapori TAWA, TFS, Wizara ya Ardhi na Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika Mkoa wa Katavi, kubaini changamoto zilizojitokeza.
“Kamati imekamilisha kazi yake na kuwasilisha taarifa ambayo serikali imetafakari na kutoa maelekezo na msimamo wake, kwa kila pori la akiba, “ameagiza Naibu Waziri Masanja
Amesema katika mapori matano yaliyobadilishwa kuwa mapori ya akiba, pori la akiba Luganzo -Tongwe Wilaya ya Tanganyika Mkoa wa Katavi, serikali imeagiza mchakato wa uanzishwaji wa pori hilo la akiba uanze upya na ufanyike haraka sambamba na kushirikisha Wizara ya Maliasili na Utalii, Wizara ya Ardhi, Mamlaka za Serikali za Mitaa,TFS na TAWA.
Awali pori hilo lilikusudiwa kujumuisha pori tengefu la Luganzo na Msitu wa Hifadhi wa Tongwe East, lakini haikufanyika, hivyo badala yake ilichukua maeneo mengine ya ziada yakiwemo hifadhi ya Msitu wa Mpanda Line, Msitu wa Tongwe West na eneo la vijiji katika makazi ya wakimbizi Mishamo.
Hivyo Naibu Waziri Masanja amesisitiza wakati mchakato huo wa kutathmini upya ukiendelea, eneo hilo lisimamiwe kwa pamoja na TAWA,TFS na Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika, Uvinza na Kaliua.