Serikali yaahidi kuboresha maslahi ya skauti

SERIKALI imeahidi kuboresha maslahi ya skauti nchini kutokana na mchango wao mkubwa katika jamii.

Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, (Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu), Patrobas Katambi ametoa ahadi hiyo bungeni, Dodoma leo Jumatano na kusema kwa sasa waliopitia skauti ni sifa ya ziada wanapojiunga na vyombo vya ulinzi na usalama na shughuli mbalimbali.

Ametoa maelezo hayo wakati akijibu maswali ya Mbunge Asha Abdallah Juma aliyetaka kujua mpango wa Serikali wa kuwanyanyua vijana waliopita Skauti kupitia ajira na ruzuku maalum kwa ajili ya kugharamia shughuli za skauti.

Akijibu maswali hayo, amesema vijana wa Skauti nchini, kama walivyo vijana wengine nchini, hupatiwa mafunzo ya ujasiri wa kutatua matatizo katika jamii, kujitolea na uzalendo.

“Kama ilivyo kwa vijana wengine wote wa Tanzania wakiwemo vijana wa skauti ambao wapo kati ya miaka 15 hadi 35, Serikali kwa kushirikiana na chama cha Skauti Tanzania imeendelea kutekeleza programu za kusaidia vijana nchini…”

Programu hizo ni kama vile klabu za skauti katika shule za msingi na sekondari ambapo vijana hupatiwa mafunzo ya ujasiri, kutatua matatizo katika jamii, kujitolea na uzalendo.

Vilevile vijana wa skauti ni miongoni mwa vijana ambao hunufaika na programu mbalimbali zinazosimamiwa na serikali ikiwa ni pamoja na fursa za mikopo yenye masharti nafuu kwa lengo la kuanzisa miradi ya uzalishaji mali inayowawezesha kujiajiri pamoja na mafunzo ya fani mbalimbali kupitia programu ya kukuza ujuzi nchini.

Habari Zifananazo

Back to top button