Serikali yaahidi Mv Liemba, Mv Mwongozo ukarabati wake kukamilika mwakani

SERIKALI imesema ifikapo Oktoba mwakani meli za Mv Liemba na Mv Mwongozo zitakuwa zimeshafanyiwa ukarabati na kuanza kutoa huduma katika Ziwa Tanganyika.

Hayo yalibainishwa jana na Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Atupele Mwakibete wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Aida Khenani (Chadema).

Katika swali lake, Khenani aliuliza kwa nini serikali isikarabati meli za zamani wakati ikisubiri kujenga meli mpya kwa ajili ya kutoa huduma katika Ziwa Tanganyika.

Akijibu swali hilo, Mwakibete alisema tayari serikali imeshatoa kazi kwa mkandarasi kuanza ukarabati wa meli hizo na zitachukua mwaka mmoja.

Hata hivyo, Mv Mwongozo ukarabati wake utachukua miezi sita na kuwahakikishia wabunge wa Rukwa, Katavi na Kigoma kuwa Oktoba mwakani meli hizo zitaanza kutoa huduma.

Alisema pia Septemba 19, ilitangazwa zabuni na itafunguliwa Novemba 11 kwa ajili ya ujenzi wa meli mpya kwa ajili ya Ziwa Tanganyika.

Katika swali lake la msingi, Khenani alitaka kufahamu lini serikali itatekeleza ahadi ya kuleta meli mbili mpya katika Ziwa Tanganyika.

Akijibu swali hilo, Mwakibete alisema serikali katika bajeti ya mwaka huu wa 2022/2023, imetenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa meli mbili mpya, chelezo na ukarabati wa meli za Mv Liemba na Mv  Sangara ili kuboresha hali ya usafirishaji katika Ziwa Tanganyika.

Alisema kati ya meli zitakazojengwa, moja ni ya kubeba abiria 600 na tani 400 za mizigo na ya pili ni ya kubeba mabehewa na malori yenye uzito wa tani 3,000.

Mwakibete alisema serikali kupitia Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL) inaendelea na mchakato wa ununuzi wa wakandarasi wa kutekeleza miradi hiyo.

 

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button