Serikali yaandaa miongozo saba kuboresha elimu

Serikali yafafanua muda mwanafunzi kukaa darasani

WIZARA ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imelieleza Bunge kuwa imeandaa miongozo kuhakikisha kuwa elimu ya awali, msingi na elimu ya ualimu zinatolewa kwa kuzingatia viwango na ubora stahiki.

Waziri wa wizara hiyo, Profesa Adolf Mkenda alisema hayo bungeni Dodoma wakati anawasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya fedha katika mwaka wa fedha 2023/24.

Profesa Mkenda alisema serikali imeandaa mwongozo wa kitaifa wa uendeshaji na viwango katika elimu ya awali Tanzania Bara kwa lengo la kuimarisha utoaji wa elimu ya awali kwa kuzingatia viwango vya ubora na kiongozi cha kutekeleza mwongozo husika.

Advertisement

Alisema pia serikali imeandaa mwongozo wa kitaifa wa uanzishaji, usimamizi na uendeshaji wa vituo shikizi vya shule ili kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji katika vituo shikizi nchini.

Profesa Mkenda alisema pia wameandaa mwongozo wa kitaifa wa uanzishaji na utekelezaji wa shughuli za ushirikiano wa wazazi na walimu katika elimu ya awali na msingi Tanzania Bara kwa lengo la kuimarisha ushirikiano kati ya wazazi na walimu katika kutoa huduma stahiki kwa wanafunzi

Alisema pia serikali imeandaa mwongozo wa upimaji shirikishi wa matokeo ya ujifunzaji kwa wadhibiti ubora wa shule kwa lengo la kuwawezesha wadhibiti ubora kupima matokeo ya ujifunzaji wa wanafunzi wa elimu ya awali, darasa la kwanza na la pili.

Profesa Mkenda alisema pia wameandaa na kusambaza mwongozo wa chakula, mwongozo wa mafunzo ya ualimu kwa vitendo na mwongozo wa elimu ya kujitegemea katika vyuo vya ualimu.

“Vilevile imehuisha mwongozo wa mashindano ya michezo na sanaa,” alisema.

Profesa Mkenda alisema serikali imeendelea kuhakikisha elimu inayotolewa katika ngazi ya awali, msingi na sekondari inaendana na mahitaji ya sasa.

Aliwaeleza wabunge kuwa imekamilisha uandishi wa mihtasari 70 katika ngazi ya elimu ya awali, msingi, sekondari kidato cha 1 – 6.

“Vilevile, imekamilisha uandishi wa aina 64 za vitabu vya sekondari kidato cha 1 – 6 kwa masomo ya sayansi, sanaa, biashara na kilimo. Aidha, imekamilisha uandishi wa aina 35 za vitabu vya kiada kwa masomo ya ufundi ngazi ya sekondari kidato cha 1 – 4,” alisema Profesa Mkenda.

Alisema serikali imekamilisha uandishi wa Kiongozi cha Mwalimu kwa masomo 24 ya Elimu ya Awali na Msingi Darasa la III – VI kwa shule zinazotumia Kiingereza kama lugha ya kufundishia ili kuwawezesha walimu kufundisha kwa ufanisi na umahiri.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *