SERIKALI imeanza mpango wa kuvuna fisi ikiwa ni mpango kabambe wa kukabiliana na changamoto za wanyama hao kuvamia maeneo ya makazi ya wananchi.
Hayo yamewekwa bayana bungeni Dodoma leo Ijumaa wakati wa kipindi cha Maswali na Majibu baada ya Mbunge wa Viti Maalum, Cecilia Paresso kutaka kufahamu mpango wa serikali wa kuwavuna fisi wanaovamia makazi ya wananchi na kujeruhi na kuua watu hususani katika Kata ya Endamarariek iliyopo wilayani Karatu, Arusha.
Katika majibu yake, Naibu Waziri wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Mary Masanja amesema: “Katika kukabiliana na changamoto ya fisi kuvamia maeneo ya makazi ya Wananchi hususan kwenye Kata ya Endamarariek wilayani Karatu.
“Kupitia Jeshi la Uhifadhi wilaya ya Karatu, Wizara imekuwa ikifanya msako wa fisi katika maeneo husika ambapo tangu mwaka 2019 hadi sasa jumla ya fisi saba wamevunwa.
“Wizara kupitia Jeshi la Uhifadhi pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Karatu imekuwa ikifanya msako wa fisi katika maeneo husika ambapo tangu mwaka 2019 hadi sasa jumla ya fisi saba (7) wamevunwa,” Naibu Waziri amesema.
Hata hivyo amewaelekeza askari wa uhifadhi Kanda ya Kaskazini kuanza zoezi la kusaka fisi wanaovamia makazi ya watu katika Halmashauri ya wilaya ya Karatu.
Katika majibu yake, Naibu Waziri amesema jumla ya mapango au makazi ya fisi 11 yameharibiwa katika eneo husika.
Amesema kuwa fisi wanaishi katika makundi, Wizara inaendelea kufanya msako ili kuyabaini makundi ya fisi yaliyosalia na kuyavunja ikiwa ni pamoja na kuharibu makazi yao.