SERIKALI imepeleka Sh milioni 40 kwa Serikali ya Kijiji cha Nyabange, Wilaya ya Butiama mkoani Mara, kwa ajili ya ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa na kimoja cha ofisi, kuanzisha Shule ya Sekondari Nyabange.
Akizungumza kwenye mkutano mkuu wa kijiji jana, Ofisa Mtendaji wa Kijiji hicho, Husna Juma, alisema ujenzi huo unatakiwa kutekelezwa mapema iwezekanavyo, ili wanafunzi watakaohitimu darasa la Saba Mwaka huu, waanze Kidato cha Kwanza kwenye madarasa hayo, Januari mwakani.
Diwani wa Kata hiyo, Jacob Shasha alishauri wananchi waliohudhuria mkutano huo, wajitolee kuchangia gharama za ujenzi huo, ili wapate madarasa yenye ubora na kisasa zaidi.
“Kama tulivyofanya kwenye ujenzi wa madarasa ya Covid 19, tukichangia ujenzi tutapata madarasa yenye sakafu ya vigae, dari yenye Gypsum na madirisha ya alminium yenye nondo, vinginevyo kwa hii shilingi milioni 40 tutajenga bora madarasa,” alisema Shasha.
Alitoa mchanganuo wa mahitaji yanayotakiwa kutolewa na wananchi kuwa ni roli 16 za mchanga kila moja Sh 70,000, roli 30 za mawe kila moja Sh 80,000 na roli tano za kokoto kila moja Sh 250,000 sawa na jumla ya Sh 4,520,000
Alisema kikao hicho pamoja na kutakiwa kufanya uamuzi juu ya masuala hayo ya ujenzi kuteua watu 12 kuunda kamati ya ujenzi, itakayosimamia hatua zote za ujenzi huo kuanzia ukusanyaji wa michango kwa wananchi, ununuzi wa vifaa na matumizi yake.
Baada ya majadiliano yaliyoafiki ushiriki wa wanakijiji katika ujenzi huo, Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Agostino Simon alisema kwa mujibu wa kumbukumbu zilizopo, kaya zenye uwezo wa kuchangia ujenzi huo ni 1200, hivyo iliafikiwa kila kaya ichangie Sh 4,000 tu.
Makubaliano yalifikiwa kwamba uchangiaji uanze wakati huo na mwisho uwe Septemba 20 mwaka huu, huku baadhi ya wanakijiji wakianza kutoa michango ya kaya zao baada ya kuahirishwa mkutano huo.
Awali ilielezwa na Ofisa Elimu wa kata hiyo, Mwita Ghati kuwa katika hali ya kawaida wanafunzi wa kidato cha kwanza wanahitaji vyumba vitatu vya madarasa.
Angalizo hilo lilisababisha mkutano huo kuafikiana kwamba ujenzi huo, utekelezwe sambamba na mkakati wa ujenzi wa jengo jingine lenye vyumba vinne vya madarasa, ambalo limefikia kwenye madirisha.