Serikali yabaini kusuasua utumiaji ARVs     

WAZIRI wa Afya, Ummy Mwalimu amesema kuwa kati ya watu 100 wanaoishi na virusi vya ugonjwa wa Ukimwi nchini, watano hawatumii dawa za kufubaza virusi vya ugonjwa huo (ARVs).

Alisema hayo alipotembelea zahanati ya Disunyala wilayani Kibaha katika Mkoa wa Pwani akiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Global, Peter Sand.

Ummy alisema asilimia tano ya watu hao waishio na virusi vya Ukimwi hawatumii dawa hizo, hivyo kuonesha kusuasua kwa utumiaji.

“Kumeonekana kusuasua pale wanapoona hawaumwi wanaacha na tusipokuwa makini tunaweza kurudi nyuma, tuko katika hatari ni vema watumie hata kama haumwi au hasikii maumivu asiache kutumia dawa,” alisema.

Alisema kumekuwa na ngono zembe hali ambayo inarudisha nyuma mapambano dhidi ya ugonjwa huo.

Mkurugenzi huyo wa Global Fund, Sand alisema ushirikiano na Serikali ya Tanzania ni mkubwa, hivyo wamekuja kuangalia baadhi ya miradi wanayoifadhili.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakari Kunenge alisema wamefurahi kuona kinachofanywa na mfuko na kuona utekelezaji ukoje Pwani. Wanashukuru kwa huduma kwani zimesogeza huduma za afya karibu na wananchi.

 

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button