Serikali yaeleza umuhimu ziara ya Samia China

SERIKALI imesema ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan nchini China kuanzia Novemba 2 mwaka huu ni heshima inayoonesha uhusiano mzuri baina ya nchi hizo mbili.

Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa alisema Dar es Salaam kuwa Rais Samia atakuwa kiongozi wa kwanza Afrika kwenda kuonana na Rais wa China, Xi Jinping tangu achaguliwe kwa mara ya tatu kuongoza chama kinachotawala nchi hiyo na kwamba watazungumzia maeneo ya kushirikiana.

“Rais atazungumzia namna gani ataimarisha uchumi, ataboresha zaidi maisha ya watu wake, ustawi wa jamii na mengine mengi,” alisema Msigwa.

Aliongeza kwamba uhusiano wa Tanzania na China ni wa udugu na kirafiki uliokuwepo kwa zaidi ya miaka 50 hata kabla ya uhuru.

Ubalozi wa Tanzania China jana ulieleza kuwa Wizara ya Mambo ya Nje ya China ilitoa taarifa kuwa Rais Samia atakwenda nchini humo kuanzia Novemba 2 hadi 4 mwaka huu kwa mwaliko wa Rais Xi.

Balozi wa China nchini, Chen Mingjian alisema safari hiyo ya Rais Samia itafungua ukurasa mpya wa uhusiano baina ya nchi hizo mbili.

Balozi Chen alisema kukutana kwa viongozi hao kutasaidia kukuza na kuimarisha zaidi uhusiano wa kidiplomasia.

Walisema hayo kwenye mkutano wa viongozi, wadau na mabalozi wa nchi za Afrika kujadili mikakati ya ushirikiano baina ya Tanzania na China ulioandaliwa na Kituo cha Utafiti na Maendeleo Afrika (CIP).

Balozi Chen alisema tangu Januari hadi Agosti mwaka huu, biashara kati ya Tanzania na China ilikuwa Dola za Marekani bilioni 5.176 ambayo alisema ni ongezeko la asilimia 30.7.

Mgeni rasmi katika mkutano huo, Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda wa Zanzibar, Omar Shaaban alisema ushirikiano kati ya China na Afrika hauna kikomo kwa sababu unahusisha maeneo mengi kama vile miundombinu, uwekezaji, fedha, kilimo, viwanda na mawasiliano.

“Bila shaka viongozi wetu wawili, Rais Samia Suluhu Hassan, Rais wa China, Xi Jinping, wamejikita katika kuimarisha uhusiano wetu katika kila nyanja ndani ya mfumo wa mikakati ya maendeleo ya Tanzania,” alisema Shaaban.

Alisema imani ya Afrika kwa ushirikiano kati ya China na Afrika ni matokeo ya sera nzuri na inayoweza kufikiwa ya China kwa bara hilo, ambayo msingi wake ni uaminifu, usawa, manufaa ya pande zote na maendeleo ya pamoja na yenye lengo la kujenga jumuiya yenye mustakabali wa pamoja wa wanadamu.

“Uhusiano kati ya China na Afrika umeimarishwa katika ngazi zote, kuanzia kisiasa na kiuchumi hadi kibiashara, kiutamaduni na nyanja nyinginezo. Ukitembea barabarani katika nchi yoyote ya Afrika na kuwauliza watu maoni yao kuhusu China, kuna uwezekano mkubwa zaidi wa kusema kwamba China ni nchi inayosaidia mataifa ya Afrika kufikia ukuaji wa uchumi, kuunda nafasi za kazi na kuboresha maisha ya watu,” alisema.

Mwanzilishi wa CIP, Profesa Humphrey Moshi alizungumzia ziara ya Rais Samia na kusema: “Nimefurahi yeye kwenda, ningekutana naye ningemwomba vitu viwili; cha kwanza amwombe Rais mwenzake amsaidie kuboresha reli ya Tanzania na Zambia (Tazara) iendane na usasa.”

Cha pili alisema Rais Samia amwombe Rais Xi kumjengea daraja la kuunganisha Zanzibar na Tanzania Bara kwani anaamini wanaweza na mpaka anasema hivyo, alifanya utafiti na kwamba Wachina wako tayari kusaidia kwani litasaidia kuongezeka kwa watalii.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa CIP, Omar Mjenga alisema safari hiyo ni habari njema kwa Rais Samia kwenda China kwa sababu toka mlipuko wa Covid-19 utokee hakuna kiongozi mwingine aliyefanya ziara huko.

Wakati huohuo, Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amempongeza Rais wa China, Xi Jinping kwa kuendelea kuchaguliwa na kukiongoza Chama cha Kikomunisti cha China (CPC).

Taarifa ya Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Charles Hilary jana ilieleza kuwa Dk Mwinyi alitoa pongezi hizo baada ya chama hicho kumtangaza rasmi Oktoba 23, mwaka huu kuwa Katibu Mkuu wa Kamati Kuu wa Chama cha CPC kwa mara ya tatu kukiongoza.

“Ikumbukwe Serikali ya China imekuwa na ushirikiano wa karibu na Zanzibar kuleta maendeleo kwenye nyanja mbalimbali ikiwemo ya afya, kilimo, maji safi na salama, miundombinu na elimu,” alisena Hilary katika taarifa hiyo kwa vyombo vya habari.

Aliongeza: “Uhusiano huo umejengwa tangu enzi za Rais wa kwanza wa Zanzibar, Hayati Sheikh Abeid Amani Karume na aliyekuwa Rais wa China, Mao Zedong.”

 

Habari Zifananazo

Back to top button