Serikali yaeleza utekelezaji mkataba wa Dubai World

Serikali yaeleza utekelezaji mkataba wa Dubai World

SERIKALI imesema mkataba kati ya nchi na nchi ‘Intergovernmental Agreement (IGA)’, juu ya uwekezaji katika maeneo ya bandari baina ya Serikali na kampuni Dubai World umeshasainiwa.

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Atupele Mwakibete ametoa maelezo hayo leo bungeni, Dodoma baada ya Mbunge wa Mlalo, Rashid Shangazi aliyetaka utekelezaji wa mkataba wa kibiashara kati ya Serikali na Kampuni ya Dubai World.

Akizungumzia hilo, Naibu Waziri amelieleza Bunge kuwa mkataba huo unaweka msingi wa serikali za pande mbili kuanza majadiliano kuhusu maeneo ya uwekezaji.

Advertisement

“Baada ya kusainiwa kwa mkataba huo, majadiliano yataendelea kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za nchi, ili kuhakikisha kwamba, uwekezaji huo unakuwa na tija kwa nchi,” amesema.

Akifafanua zaidi, matarajio ya serikali ni kuwa, majadiliano hayo yatafikia tamati mwishoni mwa mwezi Desemba, 2022.

Katika swali lake la msingi, Shangazi amehoji: “Je, ni lini utekelezaji wa mkataba wa kibiashara kati ya serikali na Kampuni ya Dubai.”

Mnamo Februari, 2022, Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), ilisaini Hati ya Makubaliano (MoU) na Kampuni ya Dubai Port World (DP-World)-Umoja wa Falme za Kiarabu, kuhusu uwekezaji katika maeneo ya bandari nchini.

Aidha, mnamo 25 Oktoba, 2022 Serikali ilisaini Makubaliano na Serikali ya Dubai (Inter-Governmental Agreement – IGA).