Serikali yaeleza wahitimu mafunzo Israel wanavyotumika kuinua kilimo
Wizara ya Kilimo imeanza kuwatumia vijana waliohitimu mafunzo kwa vitendo nchini Israel kupitia programu ya Building a Better Tomorrow (BBT) na Block Farms ambapo wanapata fursa ya kuwashirikisha vijana wengine uzoefu wao kutoka nchini Israel.
Akizungumza Bungeni Dodoma leo, Alhamisi, Waziri wa Kilimo Hussein Bashe amesema hadi sasa jumla ya vijana 79 walioshiriki mafunzo nchini Israel ni miongoni mwa vijana 812 walio kwenye mafunzo ya kilimo biashara katika vituo atamizi.
“Baada ya kipindi cha mafunzo, watapata fursa ya kufanya kilimo biashara kupitia mashamba ya pamoja (block farms) chini ya programu ya BBT,” Bashe amesema.
Bashe amelazimika kutoa majibu hayo baada ya Mbunge wa Mafinga Mjini, Cosato Chumi kuitaka Wizara ya Kilimo kueleza namna ambavyo taifa linanufaika na vijana wanaopelekwa kwenye mafunzo ya kilimo Israel.
Katika utangulizi wa majibu yake, Waziri Bashe amesema Tanzania na Israel zilikubaliana kushirikiana kwa kuanzisha programu ya kutoa mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi wanaomaliza vyuo vikuu na vyuo vya kati vya mafunzo ya kilimo na mifugo nchini Israel.
“Lengo la programu hiyo ni kuongeza ujuzi na maarifa juu ya teknolojia za kisasa kwenye sekta ya kilimo. Mheshimiwa Spika, Kuanzia mwaka 2015 hadi sasa, jumla ya vijana 261 wa Kitanzania wamenufaika na mafunzo ya kilimo kupitia Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Israel (Ministry of Foreign Affairs Israel’s Agency for International Develeopment Cooperation-MASHAV) kupitia Agrostudies,” ameeleza.