Serikali yafafanua mauzo hisa za Tanga Cement

SERIKALI imetoa ufafanuzi kuhusu ununuzi wa hisa za Tanga Cement unaofanywa na Twiga Cement, kuwa umefuata taratibu za kisheria na kwamba kampuni inayopinga ununuzi huo ya Chalinze Cement imeshafutiwa usajili kwa udanganyifu.

Mawaziri watatu walijibu hoja za wabunge 23 waliochangia mjadala wa Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa fedha 2023/24 ya Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara ambao baadhi yao walipinga ununuzi huo huku wengine wakiuunga mkono.

Akihitimisha hoja yake iliyopitishwa bungeni Dodoma jana Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Dk Ashatu Kijaji alieleza kuwa hoja za wabunge hao zilijikita katika eneo la kwa nini Tume ya Ushindani (FCC) imeruhusu muungano wa kampuni za Twiga na Tanga ambazo awali zilizuiwa na Baraza la Ushindani (FTC).

Advertisement

“Jibu sahihi ni kwamba FCC haikushughulika na ombi la muungano wa kampuni mbili ambao ulizuiwa na FTC. Tunaheshimu sheria zote za nchi hii na kama waziri niliyebeba Katiba ya nchi hii nikaapa, nimeapa kuzilinda nitazilinda,” alisisitiza.

Alisema kilichofanyika ni kwamba Desemba 22, 2022 kampuni ya Scancem International DA (Scancem) – kampuni tanzu ya Heidelberg Cement AG, inayomiliki Twiga Cement inayomiliki asilimia 69, iliomba kununua asilimia 68.33 za AfriSam Mauritius Investment Holdings Limited, mmiliki wa Tanga Cement. “Taratibu zote za kisheria zilifuatwa katika kuwasilisha na kuchambua ombi hili.

Kwa mujibu wa sheria za Ushindani na kanuni zake inatoa wajibu kwa kampuni zinazotaka kuungana na kukidhi vigezo kuwasilisha maombi yao bila kujali kama maombi yao ya awali yalikataliwa au kukubaliwa,” alieleza. Dk Kijaji alitaja vigezo hivyo kuwa ni ununuzi wa hisa au mali ya kampuni inayonunuliwa na kizingiti cha mtaji wa kampuni zote mbili kama unafikia au unazidi mtaji wa Sh bilioni 3.5 na kubadilika kwa uwezo wa kiutawala.

Alifafanua kuwa ombi hilo lililoruhusiwa ni ombi jipya kwa mujibu wa sheria na kanuni lililopokelewa kwa barua yenye kumbukumbu namba CBC 127359/144 lililotolewa mbele ya FFC kwa kuzingatia takwimu za hali ya soko la saruji kwa mwaka 2022. Dk Kijaji alifafanua kuwa kwa sababu ombi hilo lilipokelewa mwaka 2022, hakukuwa na sababu ya kutumia takwimu za mwaka 2020 na hivyo kutumia takwimu za mwaka 2022.

“Natamani sana Watanzania watuelewe, ombi hili jipya lililoruhusiwa na FCC ni tofauti na lile la awali lenye kumbukumbu namba CBC 127359/136 lililowasilishwa Novemba 2, mwaka 2021,” alisema. Alisema kwa sababu ya hoja za wabunge ombi hilo lililowasilishwa Novemba 2, 2021 liliruhusiwa kwa masharti Aprili 6, 2022 kwa kuzingatia kigezo cha uwezo uliosimikwa.

“Tuliruhusu kwa sababu utawala wa soko wa kampuni mbili zilizoomba kujiunga kutumia installed capacity (kigezo kilichowekwa) ulikuwa unafikia asilimia 31.53 ambazo ni chini ya asilimia 35 ambacho ni threshold (kizingiti) cha mwisho kilichoruhusiwa kwa kampuni,” alisema.

Alisema kutokana na sheria inavyosema, haijabainisha kitumiwe kigezo kilichowekwa au kiasi cha mauzo kwa sababu sheria ya FFC ni Sheria ya kiuchumi inayoshughulika na tabia za wateja wake katika eneo walilopo. Alibainisha kuwa mchakato wa kupokea na kuchambua maamuzi ya muungano wa kampuni hizo mbili za Twiga na Tanga unaongozwa na nadharia za kiuchumi na kibiashara ikiwemo lazima kuangalia kutofautiana kwa soko.

“Kutokana na ukweli huu viashiria kutoka mwaka 2020 hadi mwaka 2022 vilibadilika.” Alitoa mfano matukio yaliyowahi kutokea huko nyuma yanayofanana na sakata hilo kuwa ni FCC Juni 10, 2021 ilizuia ombi la kampuni ya Toyota kuinunua kampuni ya CFAO Motors kutokana na mazingira kutoruhusu lakini baadaye iliruhusu. Kuhusu hoja ya suala hilo kutokuwa na uwazi, Dk Kijaji alieleza kuwa mara baada ya ombi hilo kuwasilishwa ulifanyika mchakato wa uwazi na kwa mujibu wa Kanuni za ushindani tangazo lilitolewa katika magazeti ya Daily News na HabariLEO Februari, mwaka huu.

Aidha, alisema kikao cha wadau kilichohusisha kampuni zote za wadau wa saruji na taasisi zinazowatetea walaji walishiriki. “Sasa huyu anayekuja kinyumenyume ni nani? Siri yake ni nini?” Akizungumzia kampuni ya Chalinze Cement iliyopinga FCT mchakato huo, alisema baada ya Msajili wa Kampuni kufuatilia alibaini kuwa kampuni hiyo iliwasilisha taarifa za uongo wakati wa usajili wake na kuifuta kwa mujibu wa sheria.

Alisema msajili katika ukaguzi wake alibaini kuwa kampuni hiyo iliwasilisha anuani ya kampuni ambayo haipo kwenye usajili popote nchini, anuani za wanahisa alizosajili hazipo kwenye sajili zozote ndani ya Taifa hivyo ilikuwa na wanahisa wakufikirika. “Pia mawasiliano ya simu ya mkononi sio ya mwanahisa aliyetajwa kwenye usajili huo. Msajili alitoa notisi ya kuifuta kampuni hiyo kwa mujibu wa sheria na wakurugenzi wake walipewa muda wawasilishe majibu kwanini waliwasilisha taarifa za uongo siku 30 lakini hawakutokea,” alisema.

“Mimi mwenyewe waziri niliwahi kuwaandikia hawa Chalinze Cement nije niwatembelee kiwandani kwao mpaka leo hawajajibu, jamani hawa ni akinanani. Kampuni hii imesajiliwa mchakato wa ununuzi wa Twiga na Tanga ulipoanza huko nyuma haikuwepo,” alisema.

Aliwashukuru wabunge walioonesha kuunga mkono jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan za kulinda mazingira ya uwekezaji nchini na kumuonesha picha za wawekezaji wa Chalinze. Awali, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba alisema jambo hilo ni nyeti na serikali ina maslahi nalo na kuongeza kuwa kampuni ya Tanga Cement wawekezaji wana asilimia 68 na asilimia zilizobakia ni za serikali kupitia mifuko yake ya hifadhi ya jamii.

“Nataka niwahakikishie serikali inapeleka macho yake mawili kuhakikisha kiwanda hiki hakifi kwa sababu kimebeba maslahi ya nchi, serikali na Watanzania.

Mbali na ajira hata kwenye umiliki tuna taasisi zetu hatuwezi kuruhusu kife,” alisema.

Alisema utaratibu uliopo sasa ukiachwa uendelee mwisho wa siku serikali itabeba mzigo kwani kiwanda hicho kikifa wawekezaji kwa hali ya kifedha waliyonayo hawana uwezo wa kuubeba mzigo na kuongeza kuwa hivi sasa wawekezaji wa Tanga Cement urari wao wa kifedha uko chini ya Sh bilioni 11, deni Sh bilioni 203 na ina matumizi ya ziada ya fedha yanayofikia Sh bilioni 19.