Serikali yafafanua muda mwanafunzi kukaa darasani

WIZARA ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imesisitiza kuwa mitaala ya Elimu ya Msingi na Sekondari imeweka bayana muda unaopaswa wanafunzi kusoma.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Adolf Mkenda amesema kuwa mtaala wa Elimu ya Msingi unaeleza kuwa muda wa kusoma Elimu ya Awali na Darasa la kwanza hadi la pili ni saa tatu (dakika 180) tu kwa siku.

Kila kipindi kimoja, Waziri ameongeza, kipindi kimoja ni dakika 30.

Prof Mkenda ameongeza kuwa muda wa kusoma kwa darasa la tatu hadi la saba ni saa sita (dakika 360) kwa siku na kila kipindi ni dakika 40.

“Kwa upande wa Elimu ya Sekondari muda wa kusoma ni saa 5 na dakika 20 na kipindi kimoja ni dakika 40. Aidha, kwa mwaka wanafunzi hutakiwa kusoma kwa siku 194,” amesema.

Waziri ametoa maelezo hayo Bungeni, Dodoma leo Jumanne, baada ya Mbunge wa Viti Maalum Ng’wasi Kamani kutaka kufahamu endapo Serikali imeweka katika sheria ukomo wa saa za kufundishwa wanafunzi kama ilivyoweka kisheria ukomo wa saa za kufanya kazi kwa waajiriwa.

Katika swali lake la nyongeza, Mbunge huyo alihoji iwapo Serikali inafahamu wanafunzi wanasoma muda mrefu zaidi hata kuhatarisha afya yao ya akili.

Akijibu hayo, Waziri amesema Sheria ya Elimu haijaweka ukomo wa saa za kufundisha  wanafunzi ili kutoa fursa ya mtaala kuwa nyumbufu kulingana na mahitaji maalumu ya ujifunzaji wa wanafunzi wote pamoja na mazingira ya kujifunzia na kufundishia.

Hata hivyo ameshauri wazazi kuwaandikisha watoto katika shule jirani na makazi yao ili kuepusha mwanafunzi kutoka mapema nyumbani au kuchelewa kurudi nyumbani ili watoto wapate muda zaidi ya kucheza.

Hata hivyo Waziri amesema kuna mitaala kama ya Cambridge ambayo ni vigumu kuiwekea muda lakini ameishauri sekta binafsi kujenga shule jirani na makazi ili kutatua changamoto hizo.

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x