Serikali yafanya kweli kilimo biashara

WADAU wa sekta ya kilimo wameipongeza serikali kwa kuanza kutekeleza programu ya kuwezesha ushiriki wa vijana katika kilimo biashara (BBT- YIA).

Wizara ya Kilimo imeeleza kuwa programu hiyo inatarajiwa kuongeza ajira kwa vijana kufikia milioni tatu na kuongeza ukuaji wa sekta ya kilimo hadi kufikia asilimia 10 ifikapo mwaka 2030.

Taarifa ya wizara hiyo ilieleza kuwa inaratibu uanzishwaji wa mashamba makubwa ya pamoja na kwamba mradi huo unatekelezwa nchi nzima na vijana wote wenye sifa watapata fursa ya kufanya biashara katika mnyororo wa thamani.

Advertisement

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, wizara imetambua mashamba yenye jumla ya ekari 162,492 katika wilaya za Chunya (Mbeya), Bahi na Chamwino (Dodoma), Misenyi na Karagwe (Kagera) na Uvinza na Kasulu (Kigoma).

Katika awamu ya kwanza, wizara imepanga kutoa mafunzo ya kilimo biashara kwa vijana kwa miezi mitatu katika Kituo cha Mafunzo ya Kilimo Bihawana, Dodoma kuanzia Februari 15 mwaka huu.

Taarifa ya wizara ilieleza kuwa baada ya mafunzo, wahitimu watakabidhiwa mashamba na imekaribisha maombi ya vijana Watanzania wanaoshiriki kwenye kilimo wenye umri kuanzia miaka 18-40.

Mtaalamu wa kilimo ambaye ni waziri wa zamani wa kilimo katika serikali ya Awamu ya kwanza na ya pili, Paul Kimiti alisema programu hiyo italeta mapinduzi katika sekta ya kilimo kwa kuwa itaongeza viwanda ambavyo vinahitaji bidhaa za kilimo.

Kimiti alilieleza HabariLEO jana kuwa katika miaka ya 1995 hadi 1998 akiwa Waziri wa Kilimo, alitekeleza mpango unaofanana na huo kwa kutenga mashamba katika eneo linaloitwa Nyani wilayani Kisarawe.

“Tulifanikiwa kupata chakula kingi na vijana wale walifurahia mazingira ya shambani kwa sababu tuliwajali kwa kuwapa usafiri ambao tulipewa na wenzetu wa Tazara, ushirikiano mkubwa tuliopewa na Mkuu wa Mkoa wa Pwani wakati huo, Nicodemus Banduka,” alisema.

Mwenyekiti wa Baraza la Kilimo Tanzania (ACT), Dk Jacqueline Mkindi alisema programu hiyo ni muhimu kwa kuwa taifa lina vijana wengi zaidi kuliko makundi mengine katika jamii lakini ushiriki wao katika uzalishaji katika kilimo ni mdogo.

Dk Mkindi alisema programu hiyo itatoa fursa kwa vijana kujiajiri na kuajiri wengine kwa sababu watakapofanikiwa watasaidia vijana wengine.

“Tunaipongeza serikali kwa maono hayo kwa sababu itasaidia kwa kiwango kikubwa kuondoa vijana wengi mitaani na kusaidia kupunguza tatizo la ajira nchini, kwa hivyo malengo ya kukifanya kilimo kikue kwa asilimia 10 mwaka 2030 yatatimia kutoka hali ya sasa ya asilimia nne,” alisema Mkindi.

Alisema ni muhimu programu hiyo iwe endelevu na ili ifanikiwe, ishirikishe taasisi za fedha ili vijana wapate mitaji ya kilimo cha mashamba makubwa.

Mkufunzi Mwandamizi wa Kilimo katika Chuo cha Kilimo Tengeru Arusha, Elibariki Palangyo alisema mpango huo umefungua milango ya ajira kwa vijana na utasaidia kuondoa njaa katika jamii.

“Mpango huo utawasaidia vijana kupata pesa zitakazosaidia kunyanyua uchumi wao na familia zao pamoja na taifa kwa ujumla. Serikali pia itapata kodi kutokana na mpango huo kutokana na mpango huo kuchochea ukuaji wa viwanda,” alisema Palangyo.

Palangyo alisema programu hiyo itawasaidia pia vijana walio nje ya mpango huo kwa kupata fursa ya kufanya biashara ya pembejeo za kilimo.

Mtaalamu wa kilimo na mkulima wa mpunga mkoani Morogoro, Profesa Kitojo Wetengere alishauri programu ielimishe vijana waone umuhimu wa programu hiyo ili wawe tayari kushiriki.

“Ili kuwashawishi vijana lazima kuwe na mahala pa kujifunza hususani watu waliofanikiwa katika kilimo pamoja na kuwepo kwa miundombinu ya usafiri pamoja na kuwahakikishia soko la mazao yao watakayovuna,” alisema Profesa Watengere.

Wakati akiwasilisha bungeni mapendekezo ya serikali kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2022/2023, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba alisema serikali inalenga kutengeneza ajira kwa vijana na wanawake zaidi ya milioni tatu katika sekta ya kilimo ifikapo mwaka 2025.

“Hii itafanyika kwa kuongeza eneo la umwagiliaji kufikia hekta 8,500,000, sawa na asilimia 50 ya eneo lote linalolimwa nchini ifikapo 2030. Serikali kupitia Wizara ya Kilimo itatekeleza skimu ndogo za umwagiliaji kote nchini,” alisema Dk Mwigulu.

—————————————————————–

 

Dk Mpango atoa maagizo

upandaji, ukataji miti

 

Na Sifa Lubasi, Dodoma

 

MAKAMU wa Rais, Dk Philip Mpango amesema kwa sasa suala la upandaji miti linapaswa kuwa la lazima.

Dk Mpango ameziagiza halmashauri zote zihakikishe zinafikia lengo la upandaji miti milioni 1.5 kwa mwaka kama ilivyopangwa.

Pia aliagiza Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) kupitia upya utaratibu wa leseni za ukataji miti kwa ajili ya mkaa ili kuokoa maeneo ambayo yana uoto na vyanzo vya maji.

“Kila siku tunapishana na malori ya mkaa, pikipiki na baiskeli, miti mingi ya kutengenezea mikaa inakatwa milimani na chini ndio kuna vyanzo vya maji, tukimaliza miti yote kwenye ile milima chanzo cha maji cha Dodoma Mzakwe kitakuwa hakuna maji,” alisema Dk Mpango.

Alitoa maagizo hayo wakati akiongoza upandaji miti katika Jiji la Dodoma katika maeneo ya Ihumwa na Msalato kusherehekea maadhimisho ya miaka 59 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.

“Kupanda miti si hiari ni lazima ndio uhai wa taifa, ilani ya CCM inaelekeza kila halmashauri ipande miti milioni 1.5…tupande miti sio tunakata tu hatutafika. Watanzania wenzangu tuone tumeharibu sura ya Tanzania vya kutosha, tuna wajibu wa kuijenga upya,” alisema Dk Mpango.

Alihimiza ushirikishwaji wa sekta binafsi na wafanyabiashara katika upandaji na utunzaji miti. Alisihi familia kuongeza juhudi katika upandaji miti na usafi wa mazingira.

Dk Mpango aliagiza taasisi za serikali zipande miti katika maeneo yao na kuhakikisha miti hiyo inaishi na pia viongozi wawe mfano katika upandaji na utunzaji miti kwa kuonesha kwa vitendo.

Aliagiza Jiji la Dodoma kuratibu usimamizi wa miti iliyopandwa ili kuhakikisha inaishi na kupendezesha jiji. Alilitaka lidhibiti uchomaji moto maeneo yaliyopandwa miti sanjari na kukabili changamoto ya uingizaji au upitishaji mifugo katika maeneo hayo.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Dk Selemani Jafo alisema mipango ya uhifadhi wa mazingira imeshaanza kutekelezwa ikiwamo kugawa maeneo yaliyopandwa miti kwa taasisi za serikali na binafsi ili waweze kusimamia na kuhSERIKALI imeshauriwa kuwashirikisha diaspora katika ujenzi wa miradi ya maendeleo nchini kama sehemu ya kupandisha mchango wao katika pato la taifa.

Juzi Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Stergomena Tax aliwaeleza mabalozi na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa kuwa miongoni mwa vipaumbele vya serikali ni utekelezaji wa diplomasia ya uchumi.

Dk Tax alisema hayo alipozungumza na viongozi hao katika ofisi ndogo za wizara hiyo jijini Dar es Salaam.

Mhadhiri katika Chuo cha Diplomasia Dar es Salaam, Abass Mwalimu alisema diaspora wanaweza kuongeza kiwango cha fedha wanachotuma nyumbani kwa kujiunga katika jumuiya katika nchi wanazoishi.

“Serikali inatakiwa kuzungumza na nchi wanazoishi ili kuwalegezea masharti katika taasisi za fedha, mfano Marekani na Canada zinawataka diaspora wote kufanya miamala yote kwa kutumia benki zao lakini kama serikali ikizungumza na nchi wanaweza kuruhusiwa kufanya miamala kwa kutumia benki za Tanzania,” alisema.

Mtaalamu wa Uchumi na Diplomasia, Profesa Kitojo Wetengere alisema Tanzania bado hainufaiki vya kutosha katika kuwatumia diaspora kwa ajili ya maendeleo ya nchi.

Profesa Watengere alisema serikali inapaswa kujenga uhusiano mzuri na diaspora kwa kuwasikiliza mahitaji na changamoto zinazowakabili.

“Pia serikali inatakiwa kuruhusu uraia pacha ili kuwaondolea mzigo wa kuendeleza nchi yao wakati kipato chao hakiruhusu. Kwa kuruhusu uraia pacha Watanzania hao watapata haki zote kama raia wa nchi kama ajira na haki ya kufanya kazi hivyo itawafanya kupata fedha nyingi ambazo zitawawezesha kutuma kiwango kikubwa kuja nchini,” alisema.

Mchambuzi wa Masuala ya Siasa na Uchumi, Gabriel Mwang’onda alisema serikali inapaswa kutengeneza utaratibu ili kuwezesha baadhi ya mawaziri wanaohitajika kukutana na kuzungumza na diaspora ili kuwezesha biashara, utalii na uwekezaji nchini.

Hivi karibuni wakati akihutubia katika mkutano wa Rais Samia Suluhu Hassan na mabalozi uliofanyika Zanzibar, Dk Tax alisema mchango wa diaspora umeendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka.

Kwa mujibu wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), fedha zilizotumwa na diaspora zimeongezeka kutoka dola za Marekani milioni 400 mwaka 2020 hadi dola milioni 569.3 mwaka 2022.

Dk Tax pia alisema diaspora wamewekeza Sh bilioni 3.9 katika Dhamana ya Uwekezaji Tanzania (UTT) na wamenunua nyumba zenye thamani ya Sh bilioni 2.3 nchini.