serikali yafanya uwekezaji mkubwa mazao ya mboga mboga

SERIKALI  imefanya uwekezaji mkubwa kwenye Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu (TPHPA) na kuongeza mchango wa tasnia hiyo kwenye uchumi wa nchi.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Kilimo, Anthony Mavunde aliposhiriki uzinduzi wa Kituo cha Maarifa ya mbogamboga na Matunda kilichojengwa na Taasisi ya TAHA visiwani  Zanzibar,uzinduzi uliofanywa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.Dk  Hussein Ali Hassan Mwinyi.

“Hapo awali kama Nchi tulikuwa tukipata changamoto ya mazao yetu ya ‘horticulture’ kutopata masoko ya uhakika nje ya nchi kutokana na ubora hafifu.

“Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imefanya uwekezaji mkubwa TPHPA kwa kununua mitambo ya kisasa ya zaidi ya shilingi bilioni  2  kupima usafi wa mazao hayo ili yawe kwenye kiwango cha kimataifa, hali inayotupa fursa ya kuuza mazao yetu kokote duniani.

Amesema. hatua hiyo ya ununuzi wa mitambo ya kisasa ya kuchambua sampuli za mazao, mbolea, maji na udongo imepelekea kufanikisha kupata ithibati ambayo inasaidia mazao yatakayopimwa kukidhi viwango vya masoko ya kimataifa.

Amesema, kwa sasa, mazao yote ya mbogamboga na matunda yakishapata cheti cha ubora na kiwango kutoka TPHPA yanaweza kuuzwa sehemu yeyote nje ya nchi pasipo kuwa na shaka ya ubora, hili ni jambo kubwa sana na limefungua fursa na kuongeza uhakika wa masoko kwa mazao ya wakulima wetu nchini.

Katika kufikia Ajenda 10/30, Mavunde alibainisha kuwa moja ya mkakati wa Serikali ni kuongeza mauzo ya mazao ya bustani kutoka Dola za Marekani Milioni 750 kwa mwaka hadi kufikia Dola za Marekani Bilioni 2 mwaka 2030, hatua ambayo ni vigumu kwa Serikali kuifikia pasipo kushirikiana vilivyo na sekta binafsi ikiwemo TAHA”Alisema Mavunde

Akiongea katika uzinduzi huo Waziri wa Kilimo Umwagiliaji Maliasili na Mifugo, Shamata Shaame Khamis  alieleza kuwa mahitaji ya mazao ya bustani ni makubwa Zanzibar, ukilinganisha na uzalishaji, hivyo kituo hicho cha maarifa kimekuja wakati muafaka ili kisaidie kuongeza uzalishaji na hatimaye ziada kuuzwa nje na ameahidi kuendelea kushirikiana na Wizara ya Kilimo ya Jamhuri ya Muungano Tanzania ili kubadilishana uzoefu na ujuzi katika kuimarisha kilimo cha pande zote mbili.

Naye Mtendaji Mkuu wa TAHA, Dkt. Jacqueline Mkindi alieleza kuwa tangu TAHA imeanza kutekeleza majukumu yake Zanzibar, imesaidia kupunguza utegemezi wa mazao ya bustani kutoka nje kutoka zaidi ya asilimia 80 hadi kufikia asilimia 25 mwaka 2021 na hivyo kwasasa mazao mengi ya mboga mboga na matunda yanalimwa Zanzibar tofauti na miaka kadhaa ya nyuma.

Habari Zifananazo

Back to top button