NAIBU Waziri wa Maji, Maryprisca Mahundi, amesema serikali inaendelea na mipango ya utatuzi wa kero ya maji katika Wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza.
Mahundi amesema hayo leo wakati wa ziara ya siku moja katika mradi wa maji wa Kazilamkanda.
Amesema kukatika kwa umeme katika kituo cha maji cha Chabilungo ilikuwa tatizo kwa wakazi wa Ukerewe kupata huduma hiyo.
Ameitaka Wakala wa Maji Vijijini (RUWASA) kuhakikisha wanalipa bili ya umeme ya Sh milioni 64, ambayo Ruwasa Ukerewe inadaiwa na Shirika la Umeme nchini (TANESCO).
“Naipongeza sana Ruwasa kwa kazi nzuri wanayofanya katika kuwaletea wananchi maji, Ruwasa wajitahidi sana kuwa wanalipa bili za umeme kwa wakati na hii ni kutokana na vyanzo vyetu vingi vya maji vinatumia nishati ya Umeme,” amesema Mahundi.
Ameiagiza Ruwasa Mwanza kuendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maji. Aliahidi Serikali itaendelea kuongeza upatikanaji wa maji katika wilaya ya Ukerewe, ambapo mpaka sasa upatikanaji wa maji katika wilaya hiyo ni asilimia 62.
Ameziagiza Ruwasa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira (MWAUWASA) kuja na mpango malumu wa kudhibiti upoteaji wa maji.
Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe, Denis Mwila ameiomba Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) kupunguza kodi, ili kulipia mabomba ya mradi wa maji ya Ukara.
Ameipongeza Ruwasa kwa ufungaji wa pampu mpya za maji katika kituo cha Chabilungo.
Mbunge wa jimbo la Ukerewe, Joseph Mkundi ameiomba Ruwasa kuanzisha huduma ya kulipia bili ya maji kwa mfumo wa kielekitroniki.