Serikali yafanyia kazi kilio cha tozo

SERIKALI imesema hoja za wananchi kuhusu wingi wa tozo za kielektroniki zina mantiki hivyo inazifanyia kazi.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Innocent Bashungwa, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu, Profesa Joyce Ndalichako wamesema hayo.

Mawaziri hao wakiongozwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), George Simbachawene walikuwa wakizungumza na waandishi wa habari Dodoma jana kuhusu ufafanuzi wa tozo.

Dk Mwigulu alisema chimbuko la tozo ni kuunganisha nguvu kama Watanzania ili kutekeleza baadhi ya mahitaji ya lazima zikiwamo huduma za afya na elimu.

“Kwa mfano madarasa, nyumba za walimu, ujenzi wa vituo vya afya, ununuzi wa vifaa tiba na miundombinu kama barabara hasa vijijini,” alisema Dk Mwigulu.

Alitaja majukumu mengine kuwa ni utekelezaji wa miradi mikubwa kama ujenzi wa Bwawa la Umeme la Julius Nyerere linalogharimu Sh trilioni sita na ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) ambayo hadi ikamilike itagharimu Sh trilioni 30.

Dk Mwigulu alisema Tanzania inakuwa ni nchi ya kwanza katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) kutekeleza miradi mikubwa kwa wakati mmoja.

Alitaja miradi mingine ni kuunganisha mikoa kwa mikoa, miradi ya elimu, afya, mikopo kwa wanafunzi na umeme kusambazwa vijijini.

Dk Mwigulu alisema serikali ni sikivu kwa kuwa awali tozo ya juu ilikuwa Sh 10,000, lakini baada ya malalamiko ilipunguzwa hadi Sh 7,000 na sasa Sh 4,000.

Alisema pia waliamua kuhakikisha tozo hiyo inakuwa ya kielektroniki hadi kwenye benki na si simu pekee kwani awali ilikuwa inatozwa kwa watu wenye simu tu, lakini mtu mwingine aliweza kutoa fedha kwa kutumia kompyuta mpakato bila kukatwa.

Dk Mwigulu alisema takwimu zinaonesha kuwa tangu kuanza tozo mapato yameongezeka na mwaka 2018/19 kodi ya ushuru ilikuwa ni Sh bilioni 112 na makusanyo VAT Sh bilioni 257 na mwaka 2019/20 mapato yalikuwa Sh bilioni 103 kwenye VAT ilikuwa Sh bilioni 358.

Alisema kama tozo isingekuwepo, vituo hivyo vya afya vilivyojengwa kwa takribani Sh bilioni 117 visingekuwepo na mikopo ya elimu ya juu Sh bilioni 221 isingekuwepo.

Alisema serikali mwaka huu, imeendelea tena na tozo hizo kwa sababu bado kuna mambo ya msingi kwa jinsi nchi inavyoenda kuna umuhimu wa kuyatekeleza akitolea mfano tatizo la ajira.

Alitolea mfano kila wanapomaliza darasa la saba kuna watoto 200,000 hawaendelei kidato cha kwanza na kidato cha nne wanapomaliza shule watu 300,000 hawaendelei na kidato cha tano na sita na maana yake kuna watu 500,000 kila mwaka hawaingii kwenye mfumo wa elimu.

Alisema pamoja na changamoto hizo, serikali inaendelea na majukumu ambayo haiwezi kuyaahirisha kama vile miradi ya mkakati na shughuli nyingine za uzalishaji.

Dk Mwigulu alieleza dhamira ya serikali kuendelea kupokea maoni ya wananchi kuhusu kodi na tozo mbalimbali na kuyafanyia kazi.

Alisema amepokea maoni matatu kuhusu tozo kutoka makundi mbalimbali likiwamo Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) na wataalamu binafsi ikiwamo Taasisi ya Twaweza juu ya wafanyakazi kutozwa tozo mara mbili.

“Serikali imesikia hoja hii na ni ya msingi kweli na lengo lao ni kujenga na serikali ni heshima kubwa kupokea ushauri huu tutafanyia kazi na tutatoa majibu kwenye utekelezaji. Kuweni watulivu wakati tunafanya kwenda kwenye utekelezaji kufanyia hoja hiyo. Tunashukuru sana ina mantiki wala hatupingani,” alisema Dk Mwigulu.

Aliongeza: “Nimesikia mkilalamika kuhusu kodi ya upangishaji majengo. Hii si mpya ila utekelezaji wake ndio umeanza mwaka huu. Wengine wanasema kwanini mpangaji atozwe wakati kodi yenyewe shida kuipata. Niweke sawa hii si kodi ya mpangaji, mpangaji hawajibiki anayepaswa kulipa kodi yakupangisha ni yule aliyepata mapato ya kupangisha.”

Alikiri hatua ya mpangaji kutakiwa kuipeleka kodi hiyo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ina changamoto na kuahidi kulishughulikia suala hilo na kulitolea majibu.

Alisisitiza nia ya serikali ni kuhakikisha kila anayestahili kulipa kodi analipa kwani wapo wengi wanapata mapato makubwa, lakini hawalipi kodi na kusababisha kundi dogo linalolipa kodi kuendelea kukandamizwa.

Profesa Ndalichako aliwahakikishia wafanyakazi wote nchini na kuwatoa hofu kuhusu mishahara yao inayopitia benki kukatwa tozo mara mbili pamoja na kutakiwa kulipa tozo ya mpangaji serikalini.

 

 

 

 

 

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button