Serikali yafungia mitandao inayojihusisha na ushoga

MAMLAKA nchini Tanzania katika kujaribu kulinda maadili na utamaduni wa Mtanzania, imeanza kuchukua hatua kali ikiwa ni pamoja na kufungia akaunti za mitandao ya jamii, ambazo zinachochea mapenzi ya jinsia moja.
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye ameliambia Bunge kuwa Serikali imefunga zaidi ya akaunti na tovuti 3,360 za mitandao ya kijamii zinazohamasisha ushoga au usagaji.
Kwa mujibu wa Nape, takwimu hizo ni pamoja na akaunti 12 za Twitter, akaunti za Instagram 198, akaunti za Facebook 361, tovuti 334 na vikoa 2,456 vya mashoga.
“Tumeweza kuzuia matangazo na programu zinazokuza ushoga katika vyombo vya habari vya kawaida, kwa bahati mbaya tunapitia changamoto kwa vyombo vya habari vya mtandao,” amesema Waziri Nape. “Hili pia linahitaji jamii hasa katika ngazi ya familia kuhusika moja kwa moja.”

Mbunge wa Viti Maalumu, Anatropia Theones (Chadema) ametoa changamoto kwa Serikali Bungeni kuchukua hatua za haraka kuhusu watu wanaohamasisha ndoa za jinsia moja hadharani na kupitia vyombo vya habari.
Kulingana na mbunge huyo wafuasi wa LGBT wameachwa huru licha ya serikali kutunga sheria za kuadhibu. Alipendekeza kuwa serikali irekebishe sheria zilizopo ili kuhakikisha wale wanaojihusisha, (wenye dalili) na wale wanaofikiria kuhamasisha ushoga wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria.
“Serikali ifanye marekebisho katika sheria za nchi ili kila anayejihusisha, mwenye dalili na anayefikiria kujihusisha na mapenzi ya jinsia moja achukuliwe hatua ili kulinda maadili ya Taifa.
“Sheria iko wazi kuzuia mapenzi ya jinsia moja lakini watu wamekuwa wakijitangaza na kujinasibu kujihusisha na mapenzi ya jinsia moja,bila kuchukuliwa hatua,” Anatropia amesema bungeni leo Aprili 17, 2023 wakati wa kipindi cha maswali.
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Pauline Gekul amesema Sheria zipo zinafanya kazi na tayari wahusika wanaotiwa hatiani wameanza kutumikia vifungo vya zaidi ya miaka 30 jela.
“Tumekuwa tukichukua hatua na suala hili ni la jamii,” Gekul amesema na kusisitiza kuwa sheria zinafanya kazi.