Serikali yahimiza kilimo cha maparachichi

WAKULIMA nchini wametakiwa kujikita katika kilimo cha maparachichi ambapo utafiti uliofanywa unaonesha kwamba zao hilo linastawi na linaweza kukidhi mahitaji ya kibiashara.

Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo, Shamata Shaame Khamis alisema hayo akijibu swali la Mwakilishi wa Jimbo la Ziwani, Suleiman Makame aliyetaka kujua juhudi zilizofanywa na wizara katika kuhamasisha kilimo cha parachichi zimefikia wapi.

Shaame alisema Wizara ya Kilimo ilifanya utafiti katika mwaka 1990 katika baadhi ya mazao kuingia katika soko la kimataifa la biashara na kubainika kwamba maparachichi yanaweza kuleta mageuzi makubwa kwa wakulima.

Alisema kazi kubwa inayofanywa na taasisi za utafiti ikiwamo kilimo ni kubaini uwezekano wa mazao mengi zaidi ambayo yatawanufaisha wakulima kibiashara.

”Tulifanya utafiti mwaka 1990 na kubaini kwamba kilimo cha mazao ya parachichi kinaweza kuleta mageuzi makubwa ya kibiashara na kuingiza fedha za kigeni,” alisema.

Aliwataka wakulima kuhakikisha wanajikita katika kilimo cha maparachichi ambacho utafiti wake unaonesha kinaweza kuwakomboa wakulima kibiashara zaidi na kupata kipato cha uhakika.

Alisema soko la uhakika la maparachichi lipo katika nchi za Asia na Ulaya. ”Wenzetu wa China wametuahidi soko la uhakika la zao la parachichi ambapo huu ni wakati mwafaka kwa wakulima wetu kutumia fursa hiyo,” alisema.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button