Serikali yahimiza uwekezaji sekta ya mifugo

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki ameihimiza sekta binafsi nchini kuwekeza katika sekta ya mifugo kwa sababu kuna fursa kubwa ya kukuza mitaji yao na kupata faida.

Alitoa wito huo alipotembelea na kukagua maendeleo ya kiwanda cha kuchakata maziwa na chakula cha mifugo cha Kahama Fresh kilichopo Wilayani Karagwe, Mkoani Kagera.

“Niseme tu kwamba sisi Wizara ya Mifugo tuko tayari kumuunga mkono mwekezaji yeyote atakayeweza kufanya uwekezaji mahiri kama alivyofanya Kahama Fresh ili shughuli ya ufugaji iwe ya kibiashara zaidi na kuleta tija kwao binafsi na Taifa kwa ujumla,” alisema

Aliongeza kwa kusema kuwa wawekezaji hao binafsi wakiwekeza katika sekta ya mifugo na kufanya ufugaji wa kibiashara watasaidia kuongeza fursa za ajira kwa wananchi lakini pia watakuza pato la taifa.

Aidha, alisisitiza kuwa kupitia uwekezaji wao watasaidia Wafugaji wengine ambao wanafanya ufugaji wa kujikimu kujifunza kupitia kwao na kufanya ufugaji wenye tija kubwa zaidi.

Kwa upande wake Mwekezaji wa Kiwanda cha Kahama Fresh, Josam Mtangeki alisema kuwa wamekuwa wakipata changamoto ya maji na chakula cha mifugo hasa wakati wa kiangazi hivyo aliiomba Wizara kumuongezea eneo la lisilopungua hekta 2000 ili aweze kulima malisho kwa ajili ya mifugo yake na malisho mengine atawakopesha wafugaji wadogowadogo ambao wanamuuzia maziwa kwa ajili ya kuyachakata kiwandani hapo.

Habari Zifananazo

Back to top button