Serikali yaipongeza Yanga kuchangia damu
SERIKALI imeipongeza Klabu ya Yanga kwa kitendo cha uongozi kuhamasisha mashabiki wake na kuweza kuchangia damu kiasi cha lita 544, akisema kitendi hicho ni cha kuigwa kwani kimesaidia kuongeza kiwango cha damu katika benki ya damu ya taifa.
Alisema anakusudia kutambua rasmi mchango huo muhimu wa Yanga katika hotuba yake bungeni siku chache zijazo na kutoa wito kwa Klabu ya Simba kutengeneza hamasa kama hiyo ilI kusaidia taifa kupata damu ya kutosha.
Waziri wa Afya Ummy Mwalimu alisema hayo leo jijini Dar es Salaam alipotembelea Mpango wa Taifa wa Damu Salama kwa lengo la kuangalia hali ya upatikanaji wa damu salama nchini, kwani mahitaji ya damu ni makubwa kutokana na magonjwa na ajali zinazowakuta Watanzania.
“Naipongeza timu ya Yanga, nampongeza Rais wa Yanga Hersi Said, uongozi, wachezaji na mashabiki wa Yanga kutokana na kuchangia chupa 544 kwa siku moja. Na kwenye hotuba yangu bungeni nitatambua rasmi mchango wa Yanga,” alisema Ummy.
Aliwaomba mashabiki na uongozi wa Simba kujipanga na kutengeneza hamasa ya kuweza kuchangia damu, kwani kuchangia damu ni tendo la ibada na la huruma kuchangia damu kwa sababu itasaidia kuokoa maisha ya Watanzania.