DAR ES SALAAM: SERIKALI imesema pamoja na mafanikio kadhaa kushuhudiwa katika sekta ya elimu nchini lakini bado kuna changamoto zinazoikumba sekta hiyo.
Miongoni mwa changamoto ni kuongezeka kwa udahili wa wanafunzi ambao unahitaji ongezeko la walimu na miundombinu mingine kama madarasa na nyumba za walimu.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko leo jijini Dar es Salaam na kusema Serikali inatambua bado kuna kazi kubwa ya kufanya katika sekta ya elimu ambapo ametoa wito kwa wadau kushirikiana na Serikali ili kuimarisha mahitaji ya elimu.
Dk Biteko amesema serikali inawajali walimu nchini na ndio maana inatekeleza vipaumbele vinane ili kuboresha kada hiyo ikiwemo ujenzi wa nyumba kwenye halmashauri za pembezoni, kuimarisha mfumo wa motisha kwa walimu ili kuwafanya wabaki kwenye kazi yao, kuwezesha uandaaji wa mfumo jumuishi wa kieletroniki wa uandaaji, usimamizi na upangaji wa Walimu kwa kuzingatia usawa wa kijinsia na kuwezesha utekelezaji wa mpango wa ajira kwa walimu wa kujitolea kwa ajili ya kupungiza changamoto za upatikanaji wa walimu msingi ili kuimarisha mazingira ya kujifunza na ufundishaji.
Ametaja vipaumbele vingine kuwa, ni kumwezesha mwalimu kufanya upimaji wa kielektroniki ili kupata matokeo ya kila hatua ya kujifunza, kujenga vituo vya walimu na kuweka samani na vifaa vya kielektroniki ili kuwezesha mafunzo endelevu kwa walimu waliokazini, ununuzi wa zana na vifaa visaidizi kwa Wakufunzi, walimu, walimu tarajali na wanaofundisha wanafunzi wenye mahitaji maalumu pamoja na kutoa ufadhili wa masomo kwa walimu wanaofundisha wanafunzi wenye mahitaji maalum.