Serikali yaja na mkakati nishati safi ya kupikia
SERIKALI imetangaza dira na mkakati wa miaka 10 ya kuhamia kwenye nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 20232.
Akitangaza mkakati huo leo Novemba Mosi, 2022, Rais Samia Suluhu Hassan, amesema utaanza mwakani kwa serikali kutenga fedha za kutosha zitakazoanzisha mfuko wa nishati safi ya kupikia, lengo likiwa ni kumtua mama kuni kichwani.
“Ifikapo mwaka 2032 nataka asilimia 80 mpaka 90 ya Watanzania wawe tayari wanatumia nishati safi ya kupikia,” amesema Rais Samia.
Amemuagiza Waziri wa Nishati Januari Makamba kuhakikisha taasisi zote zinazohudumia watu zaidi ya 300 watumie nishati safi na sio mkaa kwa mwaka 2023.
“Ukiwa Wizara ya Mazingira nilikuelekeza, lakini kabla haujatekeleza ukaondoka, sasa nakuelekeza tena leo, taasisi zote kuanzia jela, mashule, vikosi vya ulinzi na usalama na taasisi nyingine zote zianze kujielekeza kwenye nishati safi, wanaweza kupelekewa gesi nakupa mwaka ujao wote, utekelezaji huo ufanyike.
“Stamico wazalishe kwa wingi mkaa ambao unatumia kidogo, mkaa safi basi utumike mkaa huo badala ya kukata miti hovyo, nataka ifikapo 2024 nisimame kwa wananchi niseme nimeweza kufanya hiki na kile,” amesema.