Serikali yajipanga kufanya sensa ya kidijiti kwa walemavu

KIGALI

RWANDA inaendelea na maandalizi kabambe ya sensa inayotumia mfumo wa  kidijiti kwa walemavu ambayo itakuwa sensa ya kwanza kuwahi kufanyika nchini kwa teknolojia ya kisasa tangu taifa lijipatie Uhuru wake miaka 60 iliyopita.

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ilisema katika taarifa kuwa takwimu za sensa hiyo inayotarajiwa kufanyika hivi karibuni zitatumika kuanzisha kanzi data ya taifa ambayo taarifa zote za watu au makundi mbalimbali zitapatikana.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, utaratibu uliokuwa ukitumika hapo mwanzo wa kutumia kalamu na karatasi katika kukusanya taarifa si rafiki katika kuanzisha kanzidata ya taifa kwa walemavu kwa kuwa kunakuwa na ugumu na changamoto kwa walemavu kushiriki katika zoezi hilo.

Baraza la Taifa la Wenye Ulemavu (NCPD), limesema kazi ya kukamilisha kazi ya sensa kwa wenye ulemavu itagharimu kiasi cha dola za Marekani milioni moja ambazo asilimia 60 ya fedha hizo zitatumika katika zoezi la kukusanya data pekee.

“Kinachoendelea sasa hivi ni upembuzi yakinifu na kufanya tathmini ya kina itakayoenda hadi Septemba na kazi rasmi ya kukusanya taarifa kuanza Oktoba mwaka huu,” ilisema taarifa ya Baraza hilo.

Baada ya kukamilisha sensa hiyo, serikali itachanganya taarifa katika Mfumo wa Kudhibiti Taarifa (DMIS) mfumo ambao ni wa kwanza kutumika Kusini mwa Jangwa la Sahara.

“Kwa sasa hatuna taarifa kamili kuhusu hali ya walemavu nchini Rwanda, tunategemea taarifa zilizokusanywa miaka zaidi ya kumi iliyopita, lakini katika ukusanyaji wa taarifa ujao tutaweza kupata taarifa ya nyumba kwa nyumba,” alisema Katibu Mkuu wa NCPD, Emmanuel Ndayisaba.

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button