Serikali kuboresha ruzuku ya pembejeo
SERIKALI imejipanga kuendelea kuboresha sekta ya kilimo kuelekea msimu mpya kwa kutoa ruzuku ya pembejeo kwa mazao yote tofauti na ilivyokuwa msimu uliopita, lengo likiwa ni kuwapunguzia changamoto wakulima.
Pia imesema hadi sasa mbolea ya kupandia imeanza kuwasili nchini na inatarajiwa kufikia Agosti 15 mwaka huu, masoko yataanza kufunguliwa maeneo mbalimbali, ili kuhakikisha wakulima wanapata kwa wakati na kuwapunguzia usumbufu kama ilivyokuwa msimu uliopita.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Kilimo Hussein Bashe Julai 30,2023 akiwasilisha taarifa yake kwa Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Abdulrahman Kinana, katika kikao cha ndani cha viongozi wa CCM Mkoa Tabora.
Amesema serikali inafahamu mwaka huu wakulima wa tumbaku hawakufurahia ruzuku,lakini msimu ujao ruzuku itakuwepo.
“Watu wote wapata ruzuku kama inavyostahili wote mtapata na kuanzia msimu huu wa kulimo, ruzuku tutaipeleka katika mazao yote ya kilimo na niwape taarifa mbolea ya kupandia tayari zimeshakuja,” amesema Bashe.
Amesema jitihada zingine serikali inazochukua ni kuendelea kutumia fursa ya uwepo wa mabonde ya maji ili kuweza kutumia fursa za maji wakati wa masika kujenga mabwawa.
“Tunafanya kila uwekezaji katika maeneo ambayo yana mabonde, ili tuweze kutumia fursa za maji wakati wa masika maji yataingia kwenye matumizi kwa kuyakinga na kujenga mabwawa. Hizo ni sehemu ya hatua ambazo serikali imechukua,” amesisitiza.
Amesema zao la tumbaku msimu huu serikali imeingiza dola za Marekani milioni 120, baada ya kuuza jumla ya kilo milioni 61 za tumbaku kutoka Mkoa wa Tabora.
“Tumeingiza dola milioni 120 ,na mpaka sasa wakulima wamelipwa dola milioni 104 bado milioni 21,” amesema Bashe.
Amesema hilo ni ongezeko kubwa tofauti na msimu wa 2021/2022 ambapo usafirishaji ulikua kilo milioni 29.
” Nitumie nafasi hii kuwambia wakulima wa Mkoa wa Tabora tumekaa na kampuni zote , kwenye changamoto ya dola tulitaka wakulima walipwe kwa shilingi lakini tukakuta tukipiga hesabu alipwe kwa shilingi halafu alipe mkopo wake kwa dola mkulima alikuwa anapoteza asilimia 20 ya mapato yake,” amesema na kuongeza:
‘Kwa hiyo tukasema kwamba ni lazima benki na kampuni ziendeele kuwalipa wakulima kwa dola ,wenye benki na kampuni wametuahidi kufikia mwanzoni mwa mwezi ujao wa nane madeni yote yatalipwa, wenye benki wametuomba tuwasaidie ili wapate dola waweze kuwalipa wakulima wa Mkoa wa Tabora, ” amesema .
Amesema serikali itahakikisha kabla ya kwenda msimu mpya wa kilimo, wakulima wa Tabora wawe wamelipwa madeni yao yote.
Kauli ya Bashe imekuja kufuatia malalamiko mengi yaliyotolewa na viongozi hao wa CCM kuhusu malipo ya tumbaku kucheleweshwa.
Akifafanua Bashe amesema, msimu huu umekuwa tofauti na misimu mingine, siku zote wakulima wa tumbaku walikuwa wanavuna tumbaku mwezi Mei masoko yanaisha mwezi wa Septemba kwa hiyo masoko yanakuwa yanatamba muda mrefu.
“Mkulima akivuna ile hasara inayotokana na kukaa muda mrefu haibebwi na kampuni , kama ulivuna mwezi wa tano unakaa na tumbaku mpaka mwezi wa nane uzito wa tumbaku unaendelea kupungua,” amesema.
Amesesma, kampuni hazipati hasara kwa sababu hiyo, kwa hiyo walibadili mfumo wa ukusanyaji.
“Tukasema ni lazima kulipa tarehe 30 mwezi wa saba masoko yote yawe yameisha ili ile hasara anayoibeba asikutane nayo….
” Niwaambie wakulima kuanzia mwaka kesho masoko yataanza mwezi wa nne na sasa tunataka kufika Juni 30 au Julai 15 masoko yote ya mwaka kesho yawe yamekwisha kwa hiyo msimu wa mkulima kukaa na tambuku utakuwa miezi miwili,” amesisitiza