DAR ES SALAAM: Serikali imesema imekamilisha mchakato wa marekebisho ya Sheria ya Huduma za Habari ya Mwaka 2016 na Kanuni zake ikiwataka wanahabari kuharakisha uundwaji wa taasisi za kusimamia sekta hiyo kwa mujibu wa Sheria.
Sheria hiyo pamoja na mambo mengine imeanzisha Bodi ya Ithibati itakayokuwa na jukumu la kutoa ithibati na vitambulisho kwa wanahabari wenye sifa. Pia inaanzisha Mfuko wa Mafunzo kwa Wanahabari na Baraza Huru la Habari Tanzania.
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amesema muda mfupi alipofanya ziara katika Kampuni ya Magazeti ya Serikali Tanzania (TSN) kuwa serikali imekamilisha mchakato na sasa ni wakati wa Wanahabari kushirikiana na Idara ya Habari (Maelezo) kukamilisha uundwaji wa taasisi hizo.
“Tumekamilisha maboresho ya Sheria na Kanuni. Tuko kwenye hatua za mwisho kuunda taasisi hizi,” amesema Waziri Nape nakuongeza kuwa “Nia ya Rais (Samia Suluhu Hassan) ni kuwa Tasnia ya Habari na wanahabari waweze kujisimamia wenyewe.”