Serikali yakamilisha mkopo wa magari 12 ya zimamoto
SERIKALI imesema imekamilisha hatua zote za mkopo wa Euro milioni 4.9 kutoka nchini Austria kwa ajili ya ununuzi wa magari 12 ya zimamoto.
Hayo yamesemwa leo Februari 8, 2023 na Naibu Waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Jumanne Sagini wakati akijibu swali la Mbunge Salim Mussa Omar wa Gando lililohoji mpango Serikali katika kuongeza magari ya kisasa ya zimamoto.
Akijibu swali hilo bungeni jijini Dodoma kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Naibu Waziri, Jumanne Sagini amesema kati ya magari hayo mawili ni ya ngazi yatakayotumika kuzima moto katika majengo marefu.
“Jeshi la Zimamoto na Uokozi linatarajia kupata magari matatu ya zimamoto yaliyopatikana kupitia bajeti ya mwaka 2020/2021 kutoka Shirika la Nyumbu ‘Tanzania Automotive Technology Centre (TATC)” amesema Waziri Sagini.