Serikali yakamilisha muswada umri wa ndoa
SERIKALI imekamilisha maandalizi ya kuandika mswada wa Sheria ya Ndoa ambayo itatoa umri wa mwanamke kuolewa, Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro.
Kumekuwa na Majadiliano ya muda mrefu kuhusu mabadiliko ya Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971, ambayo kwa muktadha imekuwa ikikinzana na Sheria ya Mtoto ambayo inamtambua mtu mwenye umri wa chini ya miaka 18 kuwa ni mtoto.
Vilevile Mahakama ya rufani ilitupa rufaa ya Serikali ya Tanzania iliyokuwa ikipinga hukumu ya Mahakama Kuu iliyobatilisha vifungu vya sheria ya ndoa ya mwaka 1971 vinavyoruhusu mtoto wa kike chini ya umri wa miaka 18 kuolewa.
Waziri wa Katiba na Sheria amemwambia Spika Dk Tulia Ackson bungeni leo Aprili 18, 2023 kuwa Serikali imekamilisha mjadala na iko tayari kuwasilisha bungeni mswada wa mabadiliko ya Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971.
Mbunge wa Viti Maalum Dk. Tea Ntala ameliambia Bunge kuwa mchakato wa kukusanya maoni umechukua muda mrefu na pia ukihusisha watu ambao wanapenda kuoa watoto wadogo na hivyo mabinti bado wanataabika.
“Swala hili limekuwa la muda mrefu na watoto wanazidi kunyanyasika,” amesema na kuhoji haja ya serikali kusitisha utaratibu wa kutafuta maoni.
Waziri wa Katiba na Sheria amefafanua kuwa baada ya Mahakama ya Rufani kutoa maamuzi, Serikali ilileta mapendekezo bungeni hata hivyo Bunge lilielekeza Serikali itafute maoni zaidi.
“Tuko tayari kuleta Mswada bungeni,” amesisitiza Dk. Ndumbaro.
Awali Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mwanaidi Ali Khamis, aliliambia Bunge kuwa Sheria ya Mtoto Na. 21 ya mwaka 2009 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2019 inatambua mtu mwenye umri chini ya miaka 18 kuwa ni mtoto hivyo ni kosa la jinai kumuhusisha na mahusiano ya kimapenzi na kumuozesha.
Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 inaruhusu mtoto wa kike kuingia kwenye ndoa akiwa na miaka 14. Serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria imeshakusanya maoni kutoka kwa wadau kuhusu upi ni umri sahihi wa kuoa na kuolewa.
“Uchambuzi wa maoni hayo umeshakamilika na yatawasilishwa ndani ya Bunge ili yajadiliwe na mabadiliko kufanyika kadri Bunge litakavyoona inafaa ili kumlinda mtoto wa kike afikie ndoto zake,” amesema Naibu Waziri.