Serikali yakamilisha safari ya Yanga Algeria

SERIKALI imeeleza kukamilisha mipango yote kwa ajili ya safari ya Yanga kuelekea Algeria kwenye mechi ya fainali ya mkondo wa pili wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya USM Alger.

Mchezo huo wa pili unatarajia kuchezwa Juni 3, mwaka huu Uwanja wa Julai 5, 1962 mjini Algiers baada ya USMA kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam juzi Jumapili.

Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa alisema kama ahadi ilivyotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan, ametekeleza kwa kutoa ndege yenye uwezo wa kubeba abiria 262 kuipeleka timu hiyo kesho Alhamisi na kurejea Julai 4, mwaka huu baada ya mechi hiyo.

“Kama ilivyotangazwa, Rais ametoa ndege ambayo ina uwezo wa kubeba abiria 262 kwa ujumla wake lakini pengine mwongozo utatolewa hapo baadaye, lakini maelekezo ya Rais Samia anahitaji ibebe wachezaji, viongozi na mashabiki wa kwenda kushangilia,” alisema Msigwa.

Alisema matokeo ya mechi ya kwanza hayakuwa mazuri lakini serikali imetekeleza wajibu wake kuhakikisha wanaondoa uchovu kwa safari ambapo ndege hiyo itaruka moja kwa moja mpaka Algiers ikitumia saa tano mpaka sita.

Alisema serikali inaamini kupitia Yanga kwamba inaweza kuuleta ubingwa huo nchini msimu huu, ndiyo maana inashirikiana nayo kuhakikisha wanatimiza ndoto yao hiyo.

Alipotafutwa Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe kufahamu kuhusiana na mipango ya safari ya timu hiyo kuelekea mchezo huo unaosubiriwa kwa hamu, simu yake ya mkononi iliita bila kupokelewa.

Wakati huo huo, Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo imetoa pole kwa familia iliyopoteza mpendwa wao, William Ernest aliyefariki katika mchezo wa kwanza wa fainali hiyo kwenye Uwanja wa Mkapa. Wizara pia ilitoa pole kwa majeruhi wengine katika tukio hilo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Wizara, inamwombea marehemu apumzike kwa amani na majeruhi wengine wapone haraka na warejee katika majukumu yao ya ujenzi wa taifa.

“Tunatoa pole kwa wafiwa na Mungu aipumzishe roho ya marehemu mahala pema peponi, lakini pia tunaombea kwa Mungu majeruhi wote wapone warejee kwenye shughuli zao za ujenzi wa Taifa,” ilisomeka taarifa hiyo ya Wizara.

Habari Zifananazo

Back to top button