Serikali yakamilisha ujenzi shule ya msingi Juhudi

SERIKALI imekamilisha ujenzi wa shule mpya ya msingi Juhudi katika mtaa wa Mwatulole mjini Geita itakayochukuwa wanafunzi 995 na kuleta ahueni ya msongamano wa wanafunzi.

Shule mpya ya Juhudi inatarajiwa kupatiwa baadhi ya wanafunzi kutoka shule za msingi Mwatulole na Nguzombili zilizopo kata ya Buhalahala mjini Geita zenye jumla ya wanafunzi 9,649.

Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Mwatulole, Catherine Mugusi amebainisha hayo mbele ya viongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa mwaka 2023 walipofika kwa ajili ya kuifungua shule hiyo.

Ameeleza, shule hiyo mpya imegharimu jumla ya Sh milioni 987.6, ambapo Halmashauri ya Mji wa Geita imetoa Sh milioni 130, Serikali Kuu Sh milioni 800, Wananchi Sh milioni 1.8 na GPE-LANES Sh milioni 55.8.

Amefafanua kuwa, miundombinu iliyojengwa na kukamilika shuleni hapo ni vyumba vya madarasa 21 pamoja na samani zake, jengo la utawala lenye ofisi nane na matundu matatu ya vyoo vya watumishi.

Ameongeza pia kuna chumba kimoja cha Tehama (Teknolojia ya Habari na Mawasiliano), matundu 40 ya vyoo vya wanafunzi, jengo moja la maktaba na nyumba pacha ya watumishi.

“Shule imepokea fedha kutoka mradi wa GPE-LANES kiasi cha Sh milioni 55.8 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa, ofisi moja, matundu sita ya vyoo vya wanafunzi wa madarasa ya awali.

“Ujenzi wa majengo yote umekamilka kwa asilimia 100 isipokuwa ujenzi wa nyumba ya mtumishi ambayo bado unaendelea pamoja na madarasa ya shule ya awali.”

Mbunge wa Jimbo la Geita mjini, Costantine Kanyasu amesema huo ni mwendelezo wa serikali ya awamu ya sita kuboresha mazingira ya ufundishaji kwa walimu na kujifunzia kwa wanafunzi wa shule za umma.

Kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa mwaka 2023, Abdallah Shaibu Kaim amefungua shule hiyo na kuwaelekeza wakandarasi kusahihisha mapungufu ya mradi huo kwa pesa zao ndani ya siku saba.

Habari Zifananazo

Back to top button