Serikali yakopeshwa tril 2.3/- za miradi

Serikali yakopeshwa tril 2.3/- za miradi

TANZANIA imesaini makubaliano ya mkopo nafuu na Serikali ya Korea Kusini wa Dola za Marekani bilioni moja sawa na shilingi trilioni 2.3 za kutekeleza miradi ya maendeleo kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia 2021 hadi 2025.

Akizungumza Alhamis Dar es Salaam wakati wa kusaini makubaliano hayo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Emmanuel Tutuba alisema fedha hizo zimetolewa kupitia Mfuko wa Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo wa Korea (EDCF).

Tutuba alitaja baadhi ya miradi ambayo imeibuliwa na iko kwenye hatua za maandalizi ya ufadhili huo kuwa ni mradi wa upanuzi wa mfumo wa Vitambulisho vya Taifa (NIDA), awamu ya pili utakaotumia Sh bilioni 163.1.

Advertisement

Mradi mwingine ni wa uboreshaji wa miundombinu ya taifa ya taarifa za ardhi utakaotumia Sh bilioni 151.5, mradi wa uendelezaji wa mifumo ya usambazaji wa majisafi na ya kutibu majitaka utakaotumia Sh bilioni 163.1.

Aidha, upo pia mradi wa ujenzi wa chuo cha Kisasa cha Mafunzo ya Usafirishaji wa Reli utakaotumia Sh bilioni 186.4 na mradi wa ujenzi wa hospitali ya Binguni, Zanzibar utakaotumia Sh bilioni 233.

Tutuba alisema miradi mingine ni ya sekta ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), miradi ya afya, nishati na miundombinu.

Alisema Tanzania na Korea Kusini ziliingia makubaliano mwaka 2004 ya kuwa na ushirikiano tangu kuanzishwa kwa mfuko wa EDCF na kuanza kutoa mkopo nafuu wa jumla wa Dola za Marekani milioni 640 kwa awamu zote tatu kuanzia mwaka 2011-2020.

Alisema katika awamu hii ya nne iliyoanza 2021 hadi 2025, mfuko umetoa jumla ya Dola za Marekani bilioni 1.64 sawa na Sh trilioni 2.3 kwa ajili ya miradi ya maendeleo na watu wa Tanzania.

“Tunawashukuru sana ndugu zetu wa Korea Kusini, wamekuwa washirika wetu wa maendeleo na wametufadhili kwenye miradi mbalimbali kama ujenzi wa daraja la Tanzanite, Dar es Salaam ambalo limebadilisha mandhari ya jiji na kupunguza msongamano wa magari kwenye eneo lile,” alisema Tutuba.

Akizungumza baada ya kusaini makubaliano hayo, Balozi wa Korea Kusini nchini, Kim Sun Pyo alisema wametoa fedha hizo katika kutekeleza makubaliano baina yao kusaidia miradi ya maendeleo.

Akizungumzia fedha hizo zitakavyosaidia miradi ya maendeleo upande wa Zanzibar, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango wa Serikali ya Zanzibar, Dk Juma Malik Akil alisema wamepata fedha za ujenzi wa Hospitali ya Binguni uliopewa Sh bilioni 233.