Serikali yakubali PPP bandari Dar, yataja sifa
SERIKALI imesema ni lazima kushirikisha sekta binafsi kuendesha Bandari ya Dar es Salaam.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa amesema hayo bungeni Dodoma wakati anajibu hoja za wabunge waliochangia makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2023/2024.
Profesa Makame Mbarawa alisema mwekezaji huyo anapaswa kuwa na uwezo wa kuiwezesha bandari hiyo ifikie ufanisi wa viwango vya kimataifa ukiwamo wa mnyororo wa usafirishaji tangu mzigo unaingizwa kwenye meli hadi unafika kwa mteja.
“Kampuni hiyo lazima iwe na mtandao mpana kupata mizigo kwenye masoko ya usafirishaji maji duniani, iwe kampuni kubwa ya kimataifa inayojulikana duniani na wawe na uwezo kimataifa kuendesha na kuendeleza shughuli za bandari,” alisema Profesa Mbarawa.
Aliwaeleza wabunge kuwa kampuni yenye sifa hizo itakapopatikana itapunguza muda wa meli kushusha mizigo kutoka siku tano hadi saa 24, kuongeza meli zinazokuja Bandari ya Dar es Salaam na itapunguza muda kushusha makasha kutoka siku nne hadi siku moja na nusu.
Alisema pia itapunguza muda wa uondoshaji mizigo kutoka saa mbili hadi kufikia dakika 30 na kufafanua, “Tunataka gari inaingia bandarini ndani ya dakika 30 inaondoka.
Tunataka kampuni ya kuongeza shehena ya mizigo kutoka tani milioni 20.
18 hadi milioni 47.57.”
Alisema kampuni yenye sifa hizo ikipatikana mapato yanayotokana na forodha yataongezeka na anataka yatoke Sh trilioni 7.56 mwaka 2022/23 hadi Sh trilioni 26.709 mwaka 2030.
“Tukifikia hapa asilimia 70 hadi 80 ya bajeti itatoka bandarini,” alisema Profesa Mbarawa.
Kwa mujibu wa Profesa Mbarawa, Sh trilioni 7.78 sawa na asilimia 37 ya mapato ya makusanyo ya forodha ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) yanatoka katika Bandari ya Dar es Salaam.
Alitaja matarajio yao mengine kwa kampuni hiyo binafsi ni kulinda ajira zilizopo na kuongeza mnyororo wa ajira mpya mpaka kufikia 28,990,000, kushuka kwa gharama za usafirishaji hivyo kusaidia kupunguza gharama za bidhaa zinazoingia nchini.
“Tunahitaji mtu wa kuchagiza sekta nyingine za usafiri kama reli, tunataka mtu wa kuleta mzigo wa kutosha kuzipa mzigo wa kutosha reli zetu tulizotumia fedha nyingi kuzijenga,” alisema.
Alisisitiza, “Suala la uwekezaji binafsi halina mjadala tunakwenda kuruhusu.”
Profesa Mbarawa alisema Bandari ya Dar es Salaam ina ushindani hasa kwenye mizigo ya Zambia, Malawi, Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na kutaja bandari za nje zinazoipa ‘presha’ ya ushindani serikali ni ya Mombasa yenye gati 17 wakati ya Dar es Salaam ina magati 12.
“Kati ya magati ya Mombasa 17, magati 13 ya mizigo ya kawaida, sita yanahudumia makasha Terminal II inaendeshwa na Mediterranean Shipping Company ya Italia, hakuna suala ya usalama inaendesha hiyo kazi. Bandari ya pili maalumu kuhudumia nafaka na inaendeshwa na sekta binafsi. Ni aibu kusema unaogopa sekta binafsi,” alisema.
“Bandari ya Beira (Msumbiji) ina magati 11 ya shehena mchanganyiko na kushushia makontena. Yote yaanaendeshwa na sekta binafsi. Ya Namibia gati yao ya makasha inaendeshwa na sekta binafsi na hakuna issue ya usalama, ni aibu kuogopaogopa,” alisema na akataja bandari iliyopo Morocco yenye magati manne ya makasha yote yakiendeshwa na sekta binafsi.