Serikali yakusanya mabilioni TAEC

DAR ES SALAAM: MAKUSANYO ya maduhuli ya Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC) yameongezeka kutoka Sh bilioni 8.7 mwaka wa fedha 2020/21 hadi kufikia Sh bilioni 10.9 kwa mwaka wa fedha 2022/23.

Akielezea mafanikio hayo leo jijini Dar es salaam, Mkurugenzi wa TAEC, Prof Lazaro Busagala amesema mafanikio hayo yamechochewa nah atua ya Serikali ya Awamu ya Sita kufungua ofisi za kanda mipakani na kutumia mifumo Tehama kama vile TANCIS, TeSWS na EDMS katika kutoa huduma.

Akiwa katika kikao kazi baina ya wahariri na waandishi wa habari kilichoandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina, Mkurugenzi huyo amesema katika utekelezaji wa sheria ya nguvu za Atom Namba 7 ya mwaka 2003, serikali imefanikiwa kusajili wataalamu wa mionzi 788 wenye sifa ya kutoa huduma ya mionzi kwa umma.

Aidha amesema ndani ya miaka mitatu, serikali imesajili wataalamu 1,289 wa kutoa huduma ya mionzi kwa wagonjwa, huku ikiendelea  kutengeneza, kukarabati na kuendesha vifaa vya nyuklia jambo ambalo halikufanikiwa kipindi cha nyuma.

Mwakilishi wa wahariri, Oscar Urassa amesema  mkutano huo umefungua uelewa zaidi wa waandishi na wahariri wa habari, hivyo itawasaidia kuwapa wananchi habari kwa kina zaidi.

TAEC imeanzishwa mwaka 2003, lengo mama ni kuhakikisha usimamizi, udhibiti na uhamasishaji wa matumizi ya amani na salama ya teknolojia ya nyuklia nchini.

Habari Zifananazo

Back to top button