Sh Bil 5 kusaidia waathirika wa Hanang
DAR ES SALAAM: SERIKALI imefanikiwa kukusanya Sh bilioni tano kwa ajili ya maafa ya maporomoko ya tope, mawe, magogo na maji kutoka mlima Hanang wilayani Hanang mkoani Manyara yaliyotokea alfajiri ya Desemba 3, mwaka huu. Sambamba na hilo, serikali imepokea misaada ya chakula, vitu na vifaa mbalimbali kutoka kwa watu binafsi, asasi, taasisi na kampuni binafsi na za umma za ndani na nje ya nchi vyenye thamani ya Sh bilioni 2.18.
Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) na Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi ilifafanua kuwa kati ya hizo Sh bilioni tano, bilioni 2.5 zilitolewa na wahisani wa nje zikipokelewa na Rais Samia Suluhu Hassan. Matinyi alisema Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Mfuko wa Maafa imekusanya Sh milioni 218.95 huku taasisi na mashirika ya umma kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina zikichangia Sh bilioni 2.23.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, idadi ya vifo haijaongezeka ikibaki 89 na majeruhi wakibaki sita ambapo watano wapo katika Rufaa ya Mkoa wa Manyara na mmoja katika Hospitali ya Wilaya ya Hanang. Matinyi alisema katika kambi za waathirika kumebaki waathirika 27 kutoka kaya 10 na wote sasa wamewekwa kwenye kambi moja ya Shule ya Sekondari Katesh. Kwa ujumla kambi tatu zilizofunguliwa zilipokea na kuhudumia waathirika 534.