Serikali yalaani mauaji ya Daktari Tarime

WIZARA ya Afya imelaani vikali kitendo cha kuuliwa kinyama kwa Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Nyangoto kilichopo Kata ya Nyamongo, Tarime Vijijini mkoani Mara,  Dk Isack Sima.

Dk Sima, ameuawa kwa kukatwakatwa na  mapanga na watu wasiojulikana wakati akitoka kituo chake cha kazi usiku wa Mei 3,2023  akirejea nyumbani.
Taarifa ya kitengo cha Mawasiliano Wizara ya Afya iliyosainiwa na Aminiel Eligaesha leo Mei 6,2023 inasema kuwa
Wizara inalaani vikali kitendo hicho cha kuuwawa kwa  mwanataaluma huyo wa udaktari.
“Tunatoa pole kwa wanafamilia na tunawaomba wawe watulivu katika  kipindi hiki Serikali kupitia vyombo mbalimbali inafanya uchunguzi wa tukio hilo na itatoa taarifa mara baada ya uchunguzi huo kukamilika. ” Amesema Eligaesha
Awali, taarifa zilizopatikana zilidai kuwa Dk Sima alikua na  kawaida  ya kujitoa kuhudumia wagonjwa hata muda wa ziada.
“Wakati anarudi nyumbani, alikutana na watu waliosimamisha pikipiki yake na kumshambulia kwa mapanga. Amekatwa kichwani, mgongoni, mikononi, miguuni yani hata haielezeki. Ameuawa kinyama,” kilieleza chanzo hicho.
Imeelezwa kuwa Dk Isack baada ya kuhitimu shahada ya udaktari Chuo Kikuu cha Mtakatifu Francisko cha Afya na Sayansi Shirikishi (SFUCHAS) na mafunzo kwa vitendo aliajiriwa kituo cha afya Nyangoto kata ya Nyamongo, Tarime vijijini ambako amefanya kazi kwa miaka miwili kama Mganga Mfawidhi.
Taarifa zinazotolewa na wananchi wa eneo hilo wanamzungumzia Dk Sima kama kijana aliyefanya kazi usiku na mchana, “Hata ukimpigia simu usiku atawasha pikipiki kuja kukuhudumia.”
Kufuatia tukio hilo, Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema anaamini  vyombo vya sheria vitachukua hatua.
Wizara ya Afya imesema inafuatilia kwa kina na aitatoa taarifa rasmi.