Serikali yanunua ng’ombe dume 366

NAIBU Waziri wa Mifugo na Uvuvi David Silinde amesema katika kipindi cha miaka miwili tangu Rais Samia Suluhu Hassan aingie madarakani, serikali imenunua madume ya ng’ombe ya kisasa 366 yenye thamani ya Silingi Milioni 878.4 ili kuboresha mifugo nchini.

Silinde ameyasema leo katika Kata ya Dakawa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro wakati wa hafla fupi ya kugawa madume 40 kwa vikundi vya wafugaji 20 ili kuboresha mifugo yao ya asili katika wilaya hiyo.

Amesema Rais Samia amekuwa akifanya kazi nzuri katika kipindi kifupi kwenye Sekta ya Mifugo akiwa na lengo la kuinua wafugaji nchini kwa kuwa na mifugo bora na kisasa.

 

Mhe. Rais anapowanyanyua wafugaji anataka wananchi kuwa na maisha bora na amekuwa akihangaika katika kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja.” Amesema Silinde

Amesema uwepo wa madume bora ya kisasa ya ng’ombe ambao wamesambazwa maeneo mbalimbali nchini, ng’ombe watakaotokana na madume hao watakuwa na nyama nyingi na kufungua fursa zaidi za upatikanaji wa nyama kwa wingi kwa ajili ya kuuza ndani na nje ya nchi.

Akimwakilisha Mkurugenzi wa Idara ya Uzalishaji na Maendeleo ya Masoko kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Afisa Mifugo Mkuu Basil Mataba amesema ng’ombe hao 366 wamegaiwa kwenye halmashauri nane katika mikoa minane ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero ambayo ina wafugaji wengi.
Mataba amebainisha kuwa licha ya ugawaji wa madume hayo kwa vikundi vya wafugaji lakini mafunzo yamekuwa yakitolewa namna ya kuwatunza na kufuatilia matumizi yake pamoja na kutatua changamoto mbalimbali ambazo zinaweza kujitokeza.

Aidha, ametoa maelekezo ya namna vikundi vinapaswa kutunza madume hayo kwa kutotumiwa katika shughuli nyingine ikiwemo ya kilimo kwa kuwa serikali imenunua na kusambaza madume kwa vikundi vya wafugaji kwa ajili ya kupandishia ng’ombe jike pekee na vikundi haviruhusiwi kuuza madume hayo.

Habari Zifananazo

Back to top button