Serikali yaokoa bil 61/- kuunganisha mifuko ya jamii

MFUKO wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) umesema serikali imeokoa zaidi ya Sh bilioni 61 za uendeshaji wa mifuko minne ya hifadhi ya jamii iliyounganishwa kuwa PSSSF iliyokuwa inatumia Sh bilioni 128 kwa mwaka.

Meneja Uhusiano kwa Umma wa PSSSF, James Mlowe, alisema tangu kuanzishwa kwa PSSSF iliyotokana na kuunganishwa kwa mifuko minne ya hifadhi ya jamii Agosti Mosi, 2018, imeendelea kuimarika kwa kulipa mafao ya wastaafu kwa mujibu wa sheria, lakini wastaafu wengi wanatapeliwa baada ya kupokea mafao yao.

Mlowe alisema hayo jana wakati maofisa wa PSSSF walipozungumza na waandishi wa habari katika kikao kazi kilichofanyika Dar es Salaam kuhusu mfuko huo.

Kikao kazi hicho kiliandaliwa na mfuko huo kwa kushirikiana na Klabu ya Waandishi wa Habari Dar es Salaam (DCPC).

Mlowe alisema serikali kabla ya kuunganisha mifuko minne (LAPF, PSPF, GEPF na PPF), ilitumia zaidi ya Sh bilioni 128 kuiendesha, lakini sasa PSSSF inatumia Sh bilioni 67 kwa mwaka kama gharama za uendeshaji.

“Kwa sasa tunawalipa wastaafu zaidi ya 150,000 kwa mwezi wastani wa shilingi bilioni 60 ukiacha mafao mengine. Lakini teknolojia pamoja na faida zake ina changamoto kubwa, wazee wetu wanaibiwa sana fedha zao za kustaafu,” alisema Mlowe.

Waliviomba vyombo vya habari kushirikiana nao kutoa elimu zaidi kwa umma dhidi ya ongezeko la matapeli wanaojinasibu kuwa ni maofisa wa serikali na kuwachukulia fedha wanachama wao wanaostaafu.

Mlowe alidai matapeli hao hutumia maendeleo ya teknolojia yaliopo sasa kupata taarifa za wastaafu na kuzitumia kuwapigia simu wakiwataka wawape fedha ili wasaidie kupata pensheni au kuwataka washiriki kwenye uwekezaji wenye faida kubwa na kuishia kutapeliwa.

Alisema matapeli hao hutafuta taarifa zao na kudai ni watumishi wa PSSSF, Hazina, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), wanawapigia na kuwatapeli wakiwataka watume fedha ili wawasaidie mambo yao.

Alisema walibaini katika ofisi za Dar es Salaam miaka kadhaa iliyopita kuwa kuna watu wanafika wanajiandikisha kama wanachama wanaotafuta msaada wa kupata madai, lakini kumbe wanazungumza na wanachama hasa wazee wanaofuatilia mafao na kuchukua namba zao wakiahidi kuwasaidia maana wanajuana na watu wakubwa na ndipo wanatapeliwa.

Alisema wastaafu na wanachama wa PSSSF wanapaswa kujua kuwa hakuna malipo ya serikali kwa sasa yanayofanyika bila namba ya udhibiti na kuzingatia hilo na wasikubali kumtumia fedha mtu anayewapigia bali watumie mifumo rasmi kupata taarifa ikiwamo kupiga simu bure 0800110040 kupata uhakika.

Ingawa hakueleza takwimu kamili za malalamiko, lakini Mlowe alisema ofisi ya PSSSF Ilala, Dar es Salaam ina malalamiko mengi ya waliopokea pensheni kutapeliwa.

Alisema ugumu wa kesi hizo ni za mtandao hivyo zinatumia muda mrefu na wengi hawapati fedha zao hivyo wamewaomba wanahabari kushirikiana nao kwa karibu kuendelea kutoa elimu kwa umma kuwa macho na matapeli hao.

Mlowe alisema mfuko huo ulipounganishwa Agosti, 2018 ulipokea deni la Sh trilioni moja kwa wastaafu na mpaka mwaka jana serikali iliwezesha kulipwa, na wanaendelea kuwalipa wanachama wanaostaafu na mafao mengine kwa wastani wa Sh bilioni 180 kila mwezi bila tatizo.

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x